Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mussa Ramadhani Sima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Primary Question

MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:- Kumekuwa na mlundikano wa madeni ya watumishi:- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuyalipa madeni hayo? (b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kuwa hakuna madeni tena?

Supplementary Question 1

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, niulize maswali madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa kila mwaka mwezi Julai kunakuwa na ongezeko la mshahara, kupanda vyeo ama madaraja kwa watumishi, lakini mpaka sasa Serikali haijafanya chochote.
Je, Serikali inatoa tamko gani kwa watumishi katika kuhakikisha kwamba hakutakuwa na mlundikano tena wa madai kwa kupandisha mishahara ya watumishi?
Pili, je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuhakikisha madai haya hayatakuwepo tena? Ahsante.

Name

Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimhakikishie tu kwamba tunaendelea kulipa madeni haya kwa kadri yanavyojitokeza na kwa kweli ukiangalia tangu mwaka 2013 tulipoanza kutumia mfumo wa taarifa za kiutumishi na mishahara, madai haya yamekuwa yakiendelea kupungua kwa nyakati mbalimbali.
Vilevile kwa upande wa madeni yanayotokana na kupandisha mishahara na kwa madeni yanayotokana na upandishwaji wa vyeo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tulishatoa maelekezo kwamba ni lazima madai haya yalipwe kupitia mfumo pindi watu hawa wanapopandishwa vyeo pamoja na madai haya yanapokuwa yamejitokeza ili kuhakikisha kwamba hatuleti milundikano ya madeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunakikisha tunakuwa na mkakati endelevu, yapo madai mengine yanatokana na watumishi kuhama, tumeshaelekeza tuhakikishe kwamba mtumishi hahamishiwi kama hakuna fedha za uhamisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, madai mengine ambayo yamekuwa yakijitokeza kwa wingi ni masuala au madai ya posho ya kukaimu. Tumeshaelekeza pia na yenyewe, pindi barua ya kukaimishwa na marekebisho ya mshahara yanapotoka, basi mtumishi aingiziwe marekebisho hayo mapema na marekebisho ya mshahara yaweze kufanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukishuhudia baadhi ya waajiri wamekuwa hawatengi fedha kwa ajili ya matibabu, likizo na posho zao nyingine, matokeo yake imekuwa inasababisha sasa pindi mtu anapotakiwa kwenda likizo, inaleta madeni makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwaagiza waajiri wote, wanapokuwa wanapanga bajeti zao za kila mwaka, wahakikishe stahili za msingi na za kisheria na za kanuni za kudumu za Utumishi wa Umma zinatengwa ili kuhakikisha kwamba hawasababishi madeni, lakini vilevile kuhakikisha tunazingatia haki za msingi za watumishi hao. Nakushukuru.