Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Primary Question

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:- Malengo ya TASAF III ni kunusuru kaya maskini hapa nchini na kutengeneza miundombinu kutokana na mahitaji na uibuaji wa kaya maskini unaofanywa na wananchi kwenye mikutano ya hadhara:- (a) Je, ni vigezo gani vinatumika kuondoa kaya zilizopendekezwa kwenye mradi na kubakiza kaya chache wakati malengo ya kaya zinazohitajika, wananchi wameshapewa tangu awali? (b) Katika Wilaya ya Kaliua, vijiji vilivyoingia kwenye miradi ni 54 tu, wakati katika vijiji vyote kuna kaya maskini sana. Je, ni lini Serikali itapeleka Mpango wa TASAF III kwenye vijiji vilivyobakia kwenye Wilaya hiyo?

Supplementary Question 1

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijauliza swali, jibu lililotolewa kwenye swali namba (b) siyo kweli kwamba Wilaya ya Kaliua imepewa asilimia 70; Wilaya ya Kaliua ina vijiji 101, vilivyopewa ni 54 tu. Kwa hiyo, ni chini ya asilimia 70 kama asilimia 55. Kwa hiyo, kama lengo ni asilimia 70, Kaliua haijapata asilimia 70 kwa hiyo, tunaomba Serikali iliangalie hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali namba moja, mchakato mzima alioeleza Mheshimiwa Waziri, kuhusiana na namna ya kuweza kupata hizi kaya maskini ni kinadharia zaidi kuliko hali halisi kule kwenye vijiji. Kama ilikuwa inafuatwa kama ilivyoandikwa hapa, isingewezekana kwamba leo hii baadhi ya Watendaji familia zao zimewekwa kwenye mpango, wenye uwezo mzuri wamewekwa kwenye mpango, maskini kabisa wameachwa.
Kwa hiyo, naomba kujua Serikali kwa kuwa hapa imeandika vizuri, imeweka utaratibu gani basi, mpango mzuri kuhakikisha haya yaliyoandikwa kwenye suala namba „A‟ yanakwenda mpaka chini kwenye ground ili wale walengwa waweze kunufaika na mradi huu wa TASAF III. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; TASAF III inalenga zaidi kutoa fedha kuliko kuweka mfumo ambao utakuwa endelevu; na kwa kuwa mpango wowote kwa kuwa ni mradi, una muda wake; naomba kujua Serikali imejiandaa vipi baada ya Mradi wa TASAF III, zile familia ambazo zinapewa fedha cash haziwekewi utaratibu wa kuweza kujiendeleza, ziweze kuwa endelevu? (Makofi)

Name

Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Magdalena Sakaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusiana na kipengele (b) kwamba wamenufaika na vijiji 54 wakati wana vijiji 101. Kwa mujibu ya taarifa za Mratibu na barua ninayo ya Machi, 2015, alieleza vimesalia vijiji 17 na nitaomba tu-share pamoja kukupa orodha hiyo na baadaye tufuatilie kwa nini visiwe ni vijiji 47 na yeye alete vijiji 17?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la kwanza kwamba katika mchakato au hatua ambazo nimeelezea za upatikanaji wa fedha za TASAF, kwamba ni wa kinadharia zaidi kuliko uhalisia; ni kweli changamoto zipo, nami naomba kupitia Bunge lako Tukufu, ukiangalia mchakato mzima wa Mpango huu wa TASAF III na awamu nyingine ambazo zilitangulia unabuniwa na jamii yenyewe. Wanachokifanya TASAF kupitia uwezeshaji wa Kitaifa wanaenda tu pale kusaidia katika kutoa elimu, kuwasaidia wananchi wa eneo husika waweze kujua ni namna gani wanaibua miradi yao.
Mheshimiwa Maibu Spika, tatizo kubwa tumegundua linajitokeza katika vijana wetu ambao siyo waaminifu ambao wanapita katika kila kaya kufanya madodoso; kwa hiyo, naomba tushirikiane, mtakapoona kuna udanganyifu wowote, ziko taratibu za malalamiko. Iko fomu Na. HU1 ya malalamiko na madai. Basi wakati wowote wanakijiji wahudhurie mikutano hii inapoitishwa, lakini vile vile wanapoona kuna kaya ambayo imeorodheshwa na siyo kaya masikini sana, basi pale pale wao kupitia Mkutano wa Kijiji waweze kuchukua hatua na mtu huyo aweze kuondolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile inapokuwa orodha hii imefikishwa TASAF Makao Makuu, wanapoanza kufanya uchambuzi kupitia kompyuta, ni uchambuzi ambao unaangalia vigezo vya umaskini kwa mujibu wa Household Survey ambayo inatolewa na National Bureau of Statistics. Wakati mwingine unakuta kaya zinazofanyiwa dodoso majumbani, hawaelezi ukweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia mara nyingi kaya ambazo zinastahili kufuatwa ni zile kaya ambazo unakuta hazina hata mlo mmoja kwa siku; ni zile kaya ambazo haziwezi kumudu gharama za matibabu; ni zile kaya ambazo haziwezi kumudu huduma mbalimbali za kijamii, lakini vilevile zina watoto wengi na zinashindwa kuwapeleka shuleni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana kupitia Bunge hili tuelimishe wananchi wetu, lakini na sisi kama TASAF, tutaendelea kuto elimu hii. Wananchi wetu kwenye zile kaya wanapofanyiwa madodoso, basi waweze kutoa taarifa zenye ukweli ili waweze kunufaika. Vilevile kupitia uongozi wa vijiji, katika mikutano ile, wanapoona mara moja kuna mtu ambaye hastahili kuingizwa, basi mara moja waweze kumtoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa takwimu tulizonazo, unajikuta katika mikutano mingine wale viongozi wa vijiji wote wanawaogopa, wanajikuta hawawezi kubainisha upungufu uliopo. Kwa hiyo, naomba sana tushirikiane kwenye hili, wakati wowote nitakuwa tayari na sisi tutafanya uhakiki na kuhakikisha kwamba hatua zinachukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari tumeshaanza kuchukua hatua. Mfano, kwa upande wa Karagwe tulichukua hatua katika Kijiji cha Kibondo lakini vile vile kwa Wilaya ya Kalambo na kwenyewe tulichukua hatua dhidi ya watumishi ambao wamefanya ubadhirifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili kwamba tumejiandaa vipi kuhakikisha sasa fedha hizi zinakuwa endelevu? Ukiangalia programu hii imeanza mwaka 2000 na hii ni awamu ya tatu; mara nyingi wale wanufaika au walengwa wanatakiwa wapate huduma hii kwa miaka mitatu. Baada ya miaka mitatu tunafanya tathmini kuangalia kama wameweza kuondokana na hali ya umaskini. Kwa kweli kwa msingi mkubwa wengi takribani asilimia 52 ambao wamekuwa wakinufaika, wameweza kunufaika na kuondokana na umasikini.
Kwa hiyo, tujitahidi tuendelee kuelimisha, waweze kunifaika, maana wako wengine wamekuwa wakitisha watu kwamba fedha hizi ni za Freemason, fedha hizi sijui ni za kitu gani; na unakuta wanufaika wengine wamekuwa hawajitokezi kunufaika nazo.

Name

Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:- Malengo ya TASAF III ni kunusuru kaya maskini hapa nchini na kutengeneza miundombinu kutokana na mahitaji na uibuaji wa kaya maskini unaofanywa na wananchi kwenye mikutano ya hadhara:- (a) Je, ni vigezo gani vinatumika kuondoa kaya zilizopendekezwa kwenye mradi na kubakiza kaya chache wakati malengo ya kaya zinazohitajika, wananchi wameshapewa tangu awali? (b) Katika Wilaya ya Kaliua, vijiji vilivyoingia kwenye miradi ni 54 tu, wakati katika vijiji vyote kuna kaya maskini sana. Je, ni lini Serikali itapeleka Mpango wa TASAF III kwenye vijiji vilivyobakia kwenye Wilaya hiyo?

Supplementary Question 2

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Angellah, nilikuwa napenda niulize swali fupi la nyongeza.
Je, kumekuwa na malalamiko katika baadhi ya maeneo kwamba fedha hizi zinatumika vibaya na wahusika wanatoa majina hewa, na inasemekana Waziri aliyekuwa ana-deal na TASAF, alitumia fedha hizo vibaya kwa ajili ya kutafuta nafasi ya Urais. Uko tayari kuchunguza hilo?

Name

Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme tu kwamba malalamiko yoyote tukatakayoyapokea, tutafanya uchunguzi. Nimekuwa nikisema suala hili kuna uwazi mkubwa katika vikao mbalimbali vya vijiji na wakati wowote mtakapoona kuna matatizo, basi msisite kututaarifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami mwenyewe nimejipanga, kutokana na malalamiko mengi ambayo nimeyasikia, kwa kweli hayo majipu tutayatumbua. (Makofi)