Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Hawa Mchafu Chakoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:- Moja ya tatizo kubwa nchini ni ukosefu wa ajira kwa vijana. Serikali imeweka vipaumbele vya kuanzisha na kukuza viwanda vidogo vidogo, vya kati na vikubwa kwa lengo la kuajiri vijana wengi wa Kitanzania:- Je, Serikali ina mikakati ipi kuhakikisha azma hiyo njema inafikiwa?

Supplementary Question 1

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba nimuulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ripoti ya Nane ya World Bank kuhusu Uchumi wa Tanzania inaonesha Watanzania milioni 12 wanaishi katika umaskini wa kutupwa, wengi wao ni vijana na kila mwaka takribani vijana laki nane wanaingia katika soko la ajira. Napenda kujua Serikali ina mpango wa kuzalisha ajira ngapi kwa mwaka?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa Mkoa wa Pwani ni wa kimkatati unaounganisha kati ya Bara pamoja na Bandari za Mtwara, Dar es Salaam pamoja na Tanga, hata hivyo vijana wengi wa mkoa huu hawana ajira. Je, Serikali ina mpango gani wa kuelekeza viwanda Mkoani Pwani na ni viwanda vya aina gani? Ahsante.

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma kwa jitihada zake kubwa ambazo amekuwa akizionesha na mapenzi ya dhati aliyonayo kwa maendeleo ya vijana hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ameuliza ni mipango ipi sasa Serikali imeweka ili kuzalisha ajira zaidi. Katika majibu yangu ya msingi nilieleza wazi kabisa kwamba pamoja na kuwa nafasi nyingi za ajira zinatengenezwa ndani ya Serikali lakini Serikali imekwenda mbele zaidi kuzipa umuhimu sekta za kipaumbele ambazo zitakuwa zinachukua vijana wengi zaidi. Lengo ni kuhakikisha tunawachukua vijana wengi zaidi kwa sababu asilimia kubwa ya wanaotafuta kazi wanajikuta wako katika informal sector, formal sector yenyewe inachukua watu wachache sana. Kwa hiyo, mpango wa Serikali ni kuhakikisha inaongeza fursa zaidi za ajira ili vijana wengi waweze kupata nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta hizo za kipaumbele ni pamoja na kilimo kama nilivyosema pale awali lakini vilevile na uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo ambavyo vitakuwa ni labour intensive ili kuchukua vijana wengi zaidi. Hata katika Global Employment Trend ambayo ILO wameitoa mwaka jana inaonesha kwamba moja kati ya maeneo ambayo yanaweza yakachukua vijana wengi kwa wakati mmoja ni eneo la viwanda vidogo vidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali imeweka msisitizo na mkazo katika eneo hili na tunajenga uwezo huo ili kuona kwamba vijana wengi wanapata ajira kupitia viwanda vidogo vidogo. Pia kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) Serikali imekuwa na mikakati na mipango mbalimbali ya kuhakikisha kwamba inawasaidia wajasiriamali wadogo kuanzisha viwanda vidogo vidogo hasa vile ambavyo vina-link ya moja kwa moja na sekta ya kilimo ambapo tunapata forward and backward linkage.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anauliza Serikali ina mpango gani kwa vijana wa Mkoa wa Pwani? Katika kuongeza ajira siku zote tumekuwa tukisema moja kati ya kazi kubwa ya kwanza kabisa ambayo tunaifanya ni kuhakikisha tunawashawishi vijana wengi sana wakae katika vikundi. Kupitia katika vikundi vyao ni rahisi Serikali kuweza kuanza kusaidia kutokana na mahitaji ya maeneo husika. Kwa mfano, vijana wengi wa Mkoa wa Pwani wanafanya shughuli za uvuvi na shughuli nyingine za viwanda vidogo vidogo. Kwa hiyo, ni vyema Mheshimiwa Mbunge pamoja na ujana wake ajitahidi basi kwenda kuwahamasisha vijana wengi wakae katika vikundi ili baadaye Serikali iweze kusaidia katika uanzishwaji wa viwanda lakini vilevile na kusaidia mikopo na mitaji kwa ajili ya vijana hawa.

Name

George Malima Lubeleje

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Primary Question

MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:- Moja ya tatizo kubwa nchini ni ukosefu wa ajira kwa vijana. Serikali imeweka vipaumbele vya kuanzisha na kukuza viwanda vidogo vidogo, vya kati na vikubwa kwa lengo la kuajiri vijana wengi wa Kitanzania:- Je, Serikali ina mikakati ipi kuhakikisha azma hiyo njema inafikiwa?

Supplementary Question 2

MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mpango wa REA umesaidia sana kusambaza umeme katika vijiji vyetu, je, SIDO haiwezi kuwasaidia vijana wetu vijijini kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kukamua karanga, ufuta ili tuweze kupata mafuta kwa ajili ya kuwauzia wananchi wetu likiwemo Jimbo la Mpwapwa

Name

Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Answer

WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, maelekezo ya Serikali ni kwamba, kupitia kata na wilaya watenge maeneo ambapo miundombinu wezeshi ya umeme na maji itapelekwa pale. Pia Mamlaka ya Wilaya ibuni ni kiwanda gani kitengenezwe kwa kuangalia malighafi, nguvukazi, soko na teknolojia rahisi. Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji itawapa elimu na utaalam na inapobidi Ofisi ya Waziri Mkuu inayohusika na Uwezeshaji itaweza kuwawezesha.
Mheshimiwa Naibu Spika, niongezee majibu ya swali la Mheshimiwa Mchafu. Mkoa wa Pwani kuna viwanda vikubwa vingi vitajengwa, hilo sina tatizo nalo. Kuna viwanda vikubwa vitajengwa Mkuranga mfano kiwanda cha kutengeneza tires na vigae, hiyo sina shida nayo. Kama nilivyomjibu Mheshimiwa Lubeleje, mtengeneze maeneo kwenye kata, muangalie rasilimali zinazopatikana, tuwapelekee umeme, tuwapelekee maji halafu wataalam watawaonesha kitu gani mtafanya kulingana na hulka zenu na ubunifu mlio nao.

Name

Issaay Zacharia Paulo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Primary Question

MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:- Moja ya tatizo kubwa nchini ni ukosefu wa ajira kwa vijana. Serikali imeweka vipaumbele vya kuanzisha na kukuza viwanda vidogo vidogo, vya kati na vikubwa kwa lengo la kuajiri vijana wengi wa Kitanzania:- Je, Serikali ina mikakati ipi kuhakikisha azma hiyo njema inafikiwa?

Supplementary Question 3

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Ni kweli kuwa taifa letu lina changamoto kubwa ya ajira kwa vijana. Kwa kuwa vijana hawa wengi wako kwenye mazingira ya vijijini, ni kwa nini sasa Serikali isianzishe Jukwaa la Vijana katika Halmashauri zetu ili vijana wetu walioko vijijini na wale walioko kwenye miji midogo kama Mbulu na kwingineko waweze kujadiliana na Maafisa Uchumi, Maafisa Vijana na Maafisa Maendeleo ya Jamii changamoto na fursa zilizoko na jinsi vijana wetu wanavyoweza kupata ajira zile ambazo si rasmi kutokana na ukosefu wa ajira? Ahsante.

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka wa jana ilipitishwa sheria hapa ya uundwaji wa Baraza la Vijana ambayo lengo lake mahsusi kabisa lilikuwa ni kwenda kusaidia kuyakusanya mawazo ya vijana na kuwashirikisha vijana katika kutatua kero na changamoto mbalimbali ambazo zinawakabili. Kwa sasa Wizara ipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa kanuni ambazo zitatoa mwongozo ni namna gani Mabaraza haya yataanzishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Mabaraza haya kuanzia katika ngazi ya kata na kuja mpaka taifa itakuwa ni kusikiliza na kujadili na vilevile kuwa sehemu ya kuwasilisha Serikalini na ushauri na matatizo ya vijana. Nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na hayo yote lakini sisi kama Wizara tumeendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa Halmashauri. Kwanza kabisa, kwa kuendelea kusisitiza kwamba kila Halmashauri nchi nzima ihakikishe inaanzisha SACCOS ya vijana ambayo lengo lake kubwa ni kuhakikisha kwamba vijana hawa wanapata mikopo na mitaji kwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia mwaka 2014 Wizara pamoja na Wakuu wa Mikoa wote tulikutana hapa Dodoma. Lengo kubwa la mkutano wetu hapa Dodoma lilikuwa ni kutenga maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za vijana hasa vijana wa pembezoni kwa maana ya vijijini ili tuanzishe kitu kinachoitwa Youth Special Economic Zone ambayo itakuwa ni sehemu kwa ajili ya vijana kufanya shughuli za uzalishaji mali. Kwa hiyo, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba aendelee kutupa ushirikano, sisi tupo tayari kushirikiana na Halmashauri kutatua changamoto za vijana.