Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Rwegasira Mukasa Oscar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Primary Question

MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:- Tanzania imekuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa miaka kadhaa sasa, ambapo Watanzania wamekuwa wakijulishwa na Serikali juu ya namna ya ushiriki wa Taifa katika mtangamano huo; ushiriki bora na wenye tija hauwezi kutokana na ushiriki mzuri wa Serikali pekee na mihimili mingine ya utawala bali pia ushiriki wa wananchi kwa ngazi ya mtu mmoja mmoja na kwa namna ya pekee Mikoa inayopakana na nchi za Jumuiya hiyo ukiwemo Mkoa wa Kagera. (a) Je, kuna mkakati gani wa Serikali kumjengea mwananchi mmoja mmoja na taasisi mbalimbali kushiriki katika Jumuiya hiyo? (b) Kama mkakati huo upo; je, ni kwa vipi wataufahamu?

Supplementary Question 1

MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika nashukuru na namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania inashiriki kwenye mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kama Taifa, lakini iko haja ya kutafuta namna ambavyo Wilaya na Halmashauri ambazo zinapakana na nchi jirani zinazoshiriki kwenye Jumuiya hii kuzitumia fursa ambazo wigo wake unaishia kwenye Wilaya zinazopakana na nchi hizo.
Kwa kuwa Biharamulo inapakana na Rwanda kijiografia na kimiundombinu; na kwa kuwa wananchi wa Biharamulo kwa kushirikiana na Mbunge wao wameshazitambua fursa lakini wanahitaji nguvu ya kidiplomasia ya ngazi ya kitaifa kuhakikisha tunazichukua; je, Waziri yuko tayari kuleta nguvu ya uchumi wa kidiplomasia Biharamulo kuzungumza nasi ili tuzitumie?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, Waziri yuko tayari kuambatana na mimi akiwa pamoja na wataalamu wa diplomasia ya uchumi kutoka Wizara yake ili tukae na wataalam wa Biharamulo tuzitumie fursa hizo? Ahsante.

Name

William Tate Olenasha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba Wilaya na jamii ambazo zipo mipakani zina nafasi kubwa zaidi ya kushiriki katika fursa zinazopatikana kwa mtangamano wa Afrika Mashariki na ni kweli kabisa nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara iko tayari kabisa kuangalia ni namna gani inasaidia jamii na Wilaya zinazopakana na nchi za jirani ili kuweza kutumia fursa hizo. Naomba nimweleze tu kwamba, hilo siyo kwamba ndiyo linaanza sasa, ni kwamba kama nilivyoeleza katika swali la msingi, tayari Wizara inatoa elimu na ufahamu kwa wananchi kutambua fursa zilizopo ili waweze kuzitumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuhusu Wizara kuandamana naye ili kufika Jimboni na kuangalia hizo fursa, naomba nilichukue hili, nitamshauri Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje ili waangalie namna ya yeye au Naibu Waziri na timu yake waweze kwenda kwa Mheshimiwa Mbunge ili waweze kuangalia namna ya kutumia hizo fursa kwa ukaribu zaidi.