Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. RITTA E. KABATI (K.n.y. MHE. MGENI JADI KADIKA) aliuliza:- Tatizo la fistula limekuwa likiwakumba wanawake wengi sana hapa nchini hususan maeneo ya vijijini hali inayowasababishia kuathirika kiakili na kimwili:- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kutokomeza tatizo hili hapa nchini? (b) Kwa sasa ni hospitali moja tu ya CCBRT hapa nchini inayotoa matibabu ya tatizo na iko Dar es Salaam tu; je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka huduma hii katika mikoa mbalimbali au kanda ili wanawake wengi waweze kupata huduma hiyo?

Supplementary Question 1

MHE. RITA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri. Naomba niulize maswali mawili madogo tu ya nyongeza.
Kwa kuwa ugonjwa huu wa fistula umeleta athari sana kwa wanawake wakiwemo hata wanawake wa Iringa pamoja na Njombe, kutokana hasa na ukosefu wa vifaa vya kujifungulia na miundombinu migumu sana ambayo wanawake wamekuwa hawavifikii hata vituo vya afya wala zahanati.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba wanawake kwanza hawajifungulii majumbani na vifaa kuwepo katika zahanati na vituo vya afya hasa vilivyopo katika vijiji vyetu huko ndani kabisa?
Swali la pili, je, Serikali imebaini ni kwa kiasi gani wanawake wameathirika kutokana na ugonjwa huu wa fistula?

Name

Ummy Ally Mwalimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Answer

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, niruhusu kwanza niseme jambo moja kwa ufupi kwamba ugonjwa wa fistula ni ugonjwa ambao unasababisha kuwepo kwa tundu lisilo la kawaida kati ya uke na kibofu cha mkojo au kati ya uke na njia ya kutolea haja kubwa.
Jambo la pili ambalo ningependa kulifafanua ni kwamba, ugonjwa huu hausababishwi na laana, kurogwa au mwanamke kutembea na wanaume wengi wakati wa ujauzito. Nimeona niliseme hili kwa sababu wanawake wengi wamekuwa ni wahanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu maswali yake mawili ya nyongeza; kwamba tuna mikakati gani sasa ya kuhakikisha wanawake wanajifungulia katika vituo vya afya. Tulieleza wakati tunawasilisha bajeti yetu hapa, la kwanza ni kwamba tutaendelea kutoa elimu kwa wanawake wajawazito kuhakikisha wanahudhuria kliniki wakati wanapokuwa wajawazito na especially tutahamasisha wale wanawake wa kuanzia miezi miwili.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ambalo tutalifanya ni kuhakikisha kwamba tunaweka huduma za upasuaji wa dharura katika vituo vya afya. Nimesikiliza michango ya Waheshimiwa Wabunge wakati wa mjadala huu ambao unaendelea wa bajeti ya Serikali hasa Wabunge wa chama changu, wanawake wa Chama cha Mapinduzi, wameongea kwa sauti kubwa sana kuhusu umuhimu wa kuboresha huduma za upasuaji wa dharura.
Kwa hiyo, nataka kumthibitishia Mheshimiwa Ritta Kabati kwamba bajeti ya Wizara ya Afya inayokuja itahakikisha tunaweka vichocheo vya kuwafanya wanawake wahudhurie kliniki na nilishasema, tutatoa vifaa vya kujifungulia kwa wanawake 500,000 kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, madhara ya ugonjwa huu wa fistula. Yapo madhara ya kiafya, madhara ya kiuchumi na kijamii. Ya kiafya kama nilivyosema, mwanamke anatokwa na mkojo bila kujizuia, lakini pia haja kubwa inatoka katika njia ya uke. Kwa hiyo, hayo ni madhara ya kiafya na asilimia 85 ya wanawake ambao wanapata fistula wanapoteza watoto.
Mhehimiwa Naibu Spika, madhara makubwa ni ya kiuchumi na kijamii. Wanawake wengi wanaachwa na wanaume wao kwa sababu tu wamepata ugonjwa huo wa fistula, lakini wanawake hawa hawawezi kufanya shughuli za kujiletea maendeleo yao kwa sababu wana harufu, hawezi hata kufungua duka la maandazi au kigenge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa ambalo nataka kuwathibitishia wanawake, ugonjwa wa fistula unatibika na matibabu yake yanapatikana katika hospitali zetu. Lengo la Wizara ya Afya ni kuhakikisha wanawake hawapati fistula, lakini kama wakipata basi wapate matibabu. Kwa hiyo, katika Hospitali zetu zote za Rufaa za Mikoa tutahakikisha huduma za upasuaji wa matibabu ya fistula zinapatikana. Nakushukuru.

Name

Maria Ndilla Kangoye

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. RITTA E. KABATI (K.n.y. MHE. MGENI JADI KADIKA) aliuliza:- Tatizo la fistula limekuwa likiwakumba wanawake wengi sana hapa nchini hususan maeneo ya vijijini hali inayowasababishia kuathirika kiakili na kimwili:- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kutokomeza tatizo hili hapa nchini? (b) Kwa sasa ni hospitali moja tu ya CCBRT hapa nchini inayotoa matibabu ya tatizo na iko Dar es Salaam tu; je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka huduma hii katika mikoa mbalimbali au kanda ili wanawake wengi waweze kupata huduma hiyo?

Supplementary Question 2

MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la fistula limekuwa likiongezeka kadri miaka inavyoenda hususan maeneo ya vijijini; je, Serikali ina mpango gani wa kuelimisha wakunga wa jadi ili kupunguza tatizo la fistula na vifo vya mama na mtoto?

Name

Ummy Ally Mwalimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Answer

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Maria Kangoye, Mbunge Viti Maalum (Vijana) kwa kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri sitawatendea haki Watanzania kama sitakiri kwamba fistula inawapata wanawake walio katika hali ya chini ambao wako vijijini na kwa sababu ya uhaba wa miundombinu wa vituo vya afya, uhaba wa wataalam, pia usafiri wa kutoka pale nyumbani kwenda kituo cha afya na wanawake wa mijini ambapo kunakuwa na msongamano wa watu katika upatikanaji wa huduma za afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Kangoye anataka kujua, Serikali tutawahamasisha au tutawashirikisha vipi wakunga wa jadi ili waweze kuhakikisha kwamba na wenyewe wanashiriki katika kuokoa vifo vya akina mama wajawazito?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, asilimia 48 ya wanawake wa Tanzania bado wanajifungulia majumbani maana yake wanajifungulia kwa wakunga wa jadi. Kwa hiyo, Wizara ya Afya itaendelea kuhakikisha tunawapa elimu na kuwaelewesha kwamba wasitoe huduma za kujifungulia kwa hawa wanawake wanaowafuata; wao wawe kama ni sehemu ya rufaa. Mwanamke akienda kwa mkunga wa jadi, basi yeye ampeleke au amhamasishe kumpeleka katika kituo cha afya. Ni jambo ambalo tutalifanyia kazi, lakini pia tumekuwa tukitoa mafunzo kwa wakunga wa jadi jinsi gani ya kuwahudumia wanawake wajawazito ili tuweze kuepusha vifo vya akina mama wajawazito.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nilisema, tumeamua kuanza kutoa vifaa vya kujifungulia kwa wanawake wajawazito ili kuwa kichocheo cha wao kwenda sasa kwenye vituo vya afya vya kujifungulia badala ya kujifungulia majumbani. Ni jambo ambalo tutalipa kipaumbele. Niwathibitishie Wabunge wenzangu wanawake, mimi ni mama; nimepita labour mara mbili. Kwa hiyo, suala la uzazi salama kwa mwanamke ni suala la kipaumbele kwangu.

Name

Bahati Ali Abeid

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mahonda

Primary Question

MHE. RITTA E. KABATI (K.n.y. MHE. MGENI JADI KADIKA) aliuliza:- Tatizo la fistula limekuwa likiwakumba wanawake wengi sana hapa nchini hususan maeneo ya vijijini hali inayowasababishia kuathirika kiakili na kimwili:- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kutokomeza tatizo hili hapa nchini? (b) Kwa sasa ni hospitali moja tu ya CCBRT hapa nchini inayotoa matibabu ya tatizo na iko Dar es Salaam tu; je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka huduma hii katika mikoa mbalimbali au kanda ili wanawake wengi waweze kupata huduma hiyo?

Supplementary Question 3

MHE. BAHATI ALI ABEID: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo hili la fistula wanawake wanapolipata, huwa wanatumia pesa nyingi ili kupona. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kwa wanawake wanaopata tatizo hili wakatibiwa bure?

Name

Ummy Ally Mwalimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Answer

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Nimshukuru sana Mheshimiwa Bahati Abeid, Mbunge wa Jimbo la Mahonda kwa swali lake zuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, sera yetu ya afya inasema mwanamke mjamzito ndiye anatakiwa kupata matibabu bure; na huduma hizi za fistula especially suala la upasuaji zinafanyika baada ya siku 40 baada ya mwanamke kujifungua. Kwa hiyo, niseme tu tumelibeba. Naomba nilipokee, haliko kisera, lakini kwa sababu kama unavyosema ni jambo ambalo linawaathiri wanawake wengi hasa wa vijijini, nitashauriana na wenzangu tuone ni jinsi gani tutatoa matibabu bure kwa wagonjwa wa fistula. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru sana Hospitali ya CCBRT, wao wanatoa matibabu bure kwa wagonjwa wa fistula. Kwa hiyo, ni changamoto kwetu sisi wa Serikali pia kuhakikisha kwamba na matibabu hayo bure ya fistula yanapatikana katika Hospitali za Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa ni kwamba ule upasuaji unachukua saa sita na daktari anatakiwa ainame kwa saa sita.
Kwa hiyo, tutaangalia ni jinsi gani tutakuja na incentive package ya jinsi gani ya kutoa motisha kwa Madaktari wetu bingwa wa magonjwa ya akina mama kuwafanyia matibabu haya bure badala ya kulipia, lakini nawashakuru sana CCBRT.