Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

John Wegesa Heche

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tarime Vijijini

Primary Question

MHE. JOHN W. HECHE aliuliza:- Wakati wa kampeni ya Urais mwaka 2015, Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli aliwaahidi wananchi wa Mji wa Nyamwaga kuwa ataanzisha mchakato wa kuwalipa wazee pensheni zao kwa wakati:- Je, mpango huo muhimu utatekelezwa lini?

Supplementary Question 1

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima, wafugaji, mafundi na kila mmoja katika Taifa hili ambaye amefikia umri wa miaka 60 amelitumikia Taifa hili kwa njia mbalimbali. Wakulima ndio waliolima chakula ambacho kinaliwa na watumishi wa Serikali, kwa maana ya kwamba utumishi wao unakuwa pensionable baadaye. Wafugaji ndiyo waliofuga mifugo ambayo tunatumia maziwa, nyama na kila kitu. Wajenzi ndiyo waliojenga nyumba ambazo watumishi wa Serikali wanaishi, lakini Taifa hili limekuwa likilipa watumishi wa Serikali tu pensheni lakini watu wengine waliolitumikia Taifa hili kwa njia moja au nyingine hawalipwi pensheni na mpaka sasa Serikali imekuwa ni mchakato na nyimbo mbalimbali.
Je, Serikali inataka kutuambia kwamba hawa watu hawakuwa muhimu katika utumishi wao kwa Taifa hili ndio maana mpaka sasa hawajaanza kulipwa pensheni? (Makofi)
Swali la pili, wimbo wa mipango, michakato, maandalizi umekuwa ni wimbo wa kawaida katika nchi hii, nataka Waziri atuambie, ni lini sasa Serikali itaanza kulipa wazee hawa ili waache kuteseka, wengine mnaona wanauawa kule vijijini Usukumani huko kwamba ni wachawi kwa sababu tu hawana pesa za matumizi na wana...

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

MHE. ANTONY P. MAVUNDE - NAIBU WAZIRI (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa wananchi wote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na inathamini mchango wa kila mmoja. Serikali inafahamu na inathamini mchango wa wazee wetu walioutoa katika ujenzi wa Taifa hili katika nyanja tofauti za kiuchumi, kiutamaduni, kijamii na kisiasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhamira ya Serikali kutekeleza mpango huu kwa wazee wote ambao wametumikia Taifa hili. Nimwondoe tu hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba dhamira ya Mheshimiwa Rais na Ilani ya uchaguzi ya CCM inavyosema mpango huu utatekelezwa kwa ajili ya wale wote ambao walitoa mchango wao kwa Taifa hili bila ubaguzi wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili amezungumza ya kwamba imekuwa ikisemwa kila mara mipango, michakato na ni lini Serikali itatekeleza mpango huu. Suala hili la mpango wa pensheni kwa wazee ni suala ambalo lilikuwa linahitaji maandalizi ya kutosha na zipo taratibu ambazo zilikuwa zimekwishatekelezwa na imebaki hatua chache za kuweza kwenda kutekeleza mpango huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwondoe hofu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika mchakato huu zipo prerequisites ambazo lazima kwanza zitekelezwe na zifanyiwe kazi, huwezi kwenda tu moja kwa moja mpaka upitie katika utaratibu kwamba ni namna gani kuona mpango huu utatekelezeka. Nimtoe hofu kwamba ni dhamira ya Serikali lakini vilevile ni ahadi ya Mheshimiwa Rais na hili litatekelezeka. (Makofi)

Name

Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Primary Question

MHE. JOHN W. HECHE aliuliza:- Wakati wa kampeni ya Urais mwaka 2015, Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli aliwaahidi wananchi wa Mji wa Nyamwaga kuwa ataanzisha mchakato wa kuwalipa wazee pensheni zao kwa wakati:- Je, mpango huo muhimu utatekelezwa lini?

Supplementary Question 2

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Swali langu la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri, kuna wastaafu wengine baada ya kupewa pensheni wanapewa kila baada ya miezi mitatu na ukitazama kuna walimu wengine wastaafu na wafanyakazi wengine, kila baada ya miezi mitatu wanapewa kiasi cha shilingi 150,000/=.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba kauli ya Mheshimiwa Waziri kwamba je, pesa hizi wana mpango wowote wa kuwaongezea na je, anaonaje kama ikawa kila mwezi mkawapatia kila mwezi badala ya kuwapatia miezi mitatu?

Name

Jenista Joackim Mhagama

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Peramiho

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake la nyongeza. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu,naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimwia Mwenyekiti, dhana ya pensheni inatawaliwa na mifumo ya utekelezaji wa dhana ya hifadhi ya jamii kwa kuzingatia sheria mbalimbali za Kimataifa, sheria za nchi lakini na taratibu pia ambazo tumejiwekea ndani ya nchi yetu. Kwa hiyo, katika kila hatua ya ulipaji wa pensheni mifumo ya uchangiaji na mifumo yote ya hifadhi ya jamii, ni lazima kuwe na ushirikishwaji wa kutosha wa kuona nani afanye nini na nani awajibike katika jambo gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili kuhakikisha kwamba pensheni zinaongezeka ama mafao ya aina yoyote yanaongezeka kupitia suala zima la hifadhi ya jamii, Serikali itaendelea kushirikiana na wadau na itaendelea kutoa taarifa, ni namna gani inaboresha ama kuongeza mafao kwa namna moja au nyingine ili kuhakikisha kwamba dhana ya hifadhi ya jamii inatekelezwa ipasavyo katika nchi yetu ya Tanzania.