Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Amina Saleh Athuman Mollel

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. AMINA S. MOLLEL (K.n.y. MHE. RAISA ABDALLAH MUSSA) aliuliza:- Mfumo wa Elimu ya Tanzania kwa kiasi kikubwa haimwandai mwanafunzi kuwa mbunifu na kuweza kujiajiri:- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kubadili mfumo wetu wa elimu ili kuchochea mwanafunzi kuwa mbunifu na kuwa na uwezo wa kujiajiri? (b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha mtaala wa elimu utakaotoa mafunzo yanayozalisha ajira?

Supplementary Question 1

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza ni kwamba zipo shule za ufundi ambazo zipo katika majengo ya shule za msingi na shule za sekondari ambazo zilikuwa zikijulikana kama shule za ufundi na sekondari. Shule hizi katika miaka ya nyuma zilikuwa maarufu sana, lakini katika miaka ya hivi karibuni shule hizi umaarufu wake umepungua. Je, Serikali haioni kuwa ni wakati sasa wa kuboresha shule hizi na vyuo vya ufundi hapa nchini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Tanzania inaelekea kwenye uchumi wa viwanda na ili kuwapata vijana wenye ujuzi kukabiliana na ajira zitakazokuwepo katika viwanda hivyo tunavyovitarajia na kwa kuwa vyuo vingi vya watu wenye ulemavu vilisaidia kwa kiasi kikubwa kuwapa mafunzo watu wenye ulemavu na katika makundi hayo ya ajira tunatarajia pia kwamba kundi la watu wenye ulemavu nao pia watakuwemo katika uchumi huu wa viwanda na biashara. Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha vyuo vya ufundi mfano kama Chuo cha Yombo Dovya na vyuo vingine ili watu wenye ulemavu waweze kujiandaa kukabiliana na ajira tunapoelekea kwenye uchumi wa viwanda? Ahsante.

Name

Eng. Stella Martin Manyanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nyasa

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. La kwanza, ni kweli kwamba kumekuwa na upungufu kidogo katika baadhi ya shule zetu hasa shule za ufundi zikiwemo zile ambazo zimekuwa ni za ufundi primary pamoja na ufundi sekondari. Sisi kama Wizara suala hilo tulishaliona na kupitia bajeti yetu ya mwaka 2016/2017, Wizara imetenga fedha kwa ajili ya kuboresha shule zote za ufundi zile za zamani ambazo ni pamoja na Mtwara, Iyunga, Ifunda, Moshi, Bwiru na Musoma, nadhani nimezitaja zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa misingi hiyo tunategemea kwamba baada ya hapo na ukarabati utakaoendelea pamoja na kuweka vifaa itasaidia kuboresha. Pia tunazipitia hata zile shule za msingi ambazo zimekuwa zikitoa mafunzo ya ufundi hasa kwa vijana wanaomaliza darasa la saba ili pia waweze kupata stadi ambazo zitawasaidia katika kumudu maisha yao. Kwa hiyo, naamini kwa bajeti ya mwaka huu, kuna marekebisho mengi ambayo yatafanyika katika eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili katika suala linalohusu watu wenye ulemavu, ni kweli ulemavu siyo maana yake kushindwa kufanya kila kitu. Mimi binafsi nilishawahi kutembelea Shule ya Yombo na nikajionea matatizo wakati huo bado sijawa Naibu Waziri. Kimsingi Waziri wangu pia yuko katika msukumo mkubwa sana kuhusiana na shule za ufundi hasa zinazowahusu watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulichoamua kukifanya katika Wizara kupitia bajeti yetu ni kuona kwanza mitaala inaboreshwa kuona inakidhi kufundisha watu wenye ulemavu na kuweza kuelewa yale wanayofundishwa kwa kutumia lugha inayoendana na hali yao, lakini vilevile vifaa saidizi vinavyoendana na hali yao. Pia kuhakikisha kwamba tunaweka vifaa ambavyo vitahusika katika mafunzo. Kwa hiyo, kwa kuwa sisi wenyewe pia ni wadau wa watu wenye ulemavu naamini kuna mambo mengi yataboreshwa katika eneo hilo.