Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 3 Sitting 28 Natural Resources and Tourism Wizara ya Maliasili na Utalii 236 2016-05-25

Name

Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Primary Question

MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-
Wavunaji na watumishi wa msitu wa Taifa Sao Hill wanapata huduma za kijamii na mahitaji yao katika Jimbo la Mafinga Mjini na kwa kuwa msimu uliopita hakuna kijiji au mtaa hata mmoja uliopata kibali cha kuvuna msitu katika Jimbo hilo:-
(a) Je, Serikali iko tayari kutoa kibali cha kuvuna msitu kwa kila kijiji au mtaa ili fedha zitakazopatikana kutokana na vibali hivyo ziweze kusaidia shuguli za kuboresha huduma za jamii kama vile kuchonga madawati na kumalizia ujenzi wa zahanati?
(b) Je, Serikali iko tayari kutoa vibali vya kuvuna misitu kwa vikundi rasmi vya wajasiliamali ili kuwasaidia kukuza mitaji yao na kujipatia maendeleo ya kiuchumi?
(c) Je, ni kiasi gani cha fedha kimetolewa kama sehemu ya kurejesha hisani kwa jamii kutoka kwa kampuni ya misitu na viwanda vikubwa vya mazao ya misitu vilivyopo kwenye Jimbo la Mafinga na maeneo ya jirani?

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ugawaji wa malighafi kutoka katika mashamba ya miti unaongozwa na Mwongozo wa Uvunaji wa mwaka 2007 uliofanyiwa mapitio mwaka 2015. Aidha, Wizara yangu kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania imekuwa ikipokea na kuyafanyia kazi maombi mengi ya vibali vya uvunaji vyenye uhitaji wa mita za ujazo nyingi kuliko kiwango kinachoruhusiwa ikilinganishwa na uwezo wa mashamba wa kutoa malighafi kwa viwanda vya uchakataji wa mazao ya misitu kwa mwaka. Kwa mfano mwaka 2015/2016, jumla ya maombi 4,986 ambayo yalihitaji mita za ujazo 15,454,214 yalipokelewa na kufanyiwa kazi. Hata hivyo, ni maombi 1,030 pekee yenye jumla ya mita za ujazo 740,800 yaliidhinishwa, ambacho ndicho kiwango cha ukomo kulingana na uwezo wa mashamba katika mwaka huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uchache wa malighafi, Wizara imekuwa inatoa kipaumbele cha vibali vya uvunaji miti kwa viwanda vyenye mikataba na Serikali, miongoni mwao ni baadhi ya viwanda vya Serikali vilivyobinafsishwa, viwanda vingine vikubwa na vya kati, ikifuatiwa na wavunaji wadogo wadogo, vikundi na taasisi za watu binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imekuwa ikitoa vibali pia kwa wadau na vijiji vinavyopakana na misitu kwa ajili ya shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na utengenezaji wa madawati. Kwa mfano, katika shamba la miti la Sao Hill kati ya mwaka 2010/2011 na 2015/2016 vibali vya uvunaji kwa vijiji 183 vyenye thamani ya sh. 2,820,000,000 vilitolewa. Vile vile, shamba la Sao Hill lilihifadhili miradi ya maendeleo yenye thamani ya shilingi milioni 880 ikiwemo utengenezaji wa madawati katika vijiji 23.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uzoefu wa hivi karibuni Wizara yangu imeona haja ya kupitia upya mwongozo wa uvunaji wa mwaka 2007 kwa namna ambayo itazingatia manufaa kwa jamii jirani na misitu hiyo kama ilani ya CCM inavyoelekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu haina takwimu zinazohusu kiasi cha fedha zilizorejeshwa kama hisani kwa jamii kutoka kampuni na viwanda vikubwa vya mazao ya misitu vilivyopo kwenye Jimbo la Mafinga Mjini na maeneo ya jirani. Aidha, ushauri unatolewa kwa Mheshimiwa Mbunge awasiliane na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafinga ili aweze kupatiwa takwimu hizo.