Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 11 Sitting 32 Works, Transport and Communication Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi 425 2023-05-24

Name

Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza: -

Je, Utekelezaji wa mradi wa Mtwara Corridor umefikia hatua gani?

Name

Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Issa Malapo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Ushoroba wa Mtwara (Mtwara Corridor) unajumuisha miradi ya Sekta mbalimbali ikiwa pamoja na Madini, Uchukuzi na Kilimo. Kwa upande wa Sekta ya Uchukuzi, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imetekeleza miradi ya ujenzi wa gati kubwa na la kisasa katika Bandari ya Mtwara lenye urefu wa mita 300. Ujenzi wa Bandari ya Ndubi ambao ulikamilika tangu Desemba, 2021 na Ujenzi wa bandari mpya ya Mbamba Bay ambao upo katika hatua za manunuzi ya Mkandarasi.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali kupitia Shirika la Reli (TRC) imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kwa ajili ya ujenzi wa reli ya Standard Gauge ya Mtwara - Mbamba Bay na matawi yake kuelekea Liganga na Mchuchuma. Mradi huu unatarajiwa kutekelezwa kwa utaratibu wa ubia kati ya sekta ya Umma na sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na taarifa hizo za miradi, naomba kulifahamisha Bunge lako kuwa, gati jipya lililojengwa katika Bandari ya Mtwara limeanza kuhudumia meli za makasha pamoja na shehena ya Kichele na takriban kila baada ya wiki moja kuanzia tarehe 20/04/2023 limekuwa likihudumia mizigo ya makasha ya yanayokwenda visiwa vya Comoro.

Mheshimiwa Spika, vikao vya wadau wa Ushoroba wa Mtwara vimeanza kuratibiwa chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ili kuweka mikakati ya kuendelea kuutangaza zaidi ushoroba huo na kuwavutia wananchi waishio ukanda huo pamoja na nchi jirani kutumia Bandari ya Mtwara na kuufanya ushoroba huo kutumika ipasavyo, ahsante.