Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 8 Sitting 6 Youth, Disabled, Labor and Employment Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu 85 2022-09-20

Name

Rehema Juma Migilla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ulyankulu

Primary Question

MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuwapatia warithi wa mstaafu asilimia 67 ya michango yake pindi anapofariki?

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Ulyankulu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii hutoa mafao kwa wanachama wake kwa mujibu wa Sheria ya Hifadhi ya Jamii Sura Na. 135 kama ilivyorejewa kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria Na. 6 ya Mwaka 2019 ambapo fao la warithi ni mojawapo ya mafao yanayotolewa pindi mwanachama anapofariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Mfuko wa PSSSF, kupitia Kifungu cha 39(1) cha Sheria ya Mfuko, mstaafu anapofariki Mfuko hulipa mafao ya mkupuo ambayo ni jumla pensheni ya miezi 36 (sawa na miaka mitatu) kwa wategemezi. Kwa upande wa NSSF pia, kwa mujibu wa Kifungu cha 37(1)(2)(3) cha Sheria ya Mfuko, mstaafu anapofariki Mfuko hulipa mafao ya mkupuo sawa na pensheni ya miezi 36 kwa wategemezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ulipaji wa mafao huzingatia Sheria ya Hifadhi ya Jamii ya Mwaka 2018 na Marekebisho yake ya Mwaka 2019 na Kanuni za Mafao kama zilivyorejewa mwaka 2022. Mafao yanayolipwa hayazingatii asimilia ya michango isipokuwa wastaafu na wategemezi hulipwa mafao kwa mujibu wa kanuni zinazoongoza ulipaji wa mafao.