Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 6 Sitting 14 Industries and Trade Wizara ya Viwanda , Biashara na Uwekezaji 162 2022-02-18

Name

Timotheo Paul Mnzava

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Vijijini

Primary Question

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua Kiwanda cha Tembo Chipboard kilichopo Kata ya Mkumbara Wilayani Korogwe?

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara naomba kujibu swali la Mheshimiwa Timotheo Paul Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Tembo Chipboards Limited ni kiwanda kilichokuwa kikimilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ikiwa na hisa asilimia 80 na Kampuni ya Grewalls Saw Mills asilimia 20. Mnamo tarehe 13 Aprili, 2004 Serikali ilibinafsisha kiwanda hicho kwa kuuza hisa zake zote asilimia 80 kwa mwekezaji wa kampuni ya MELJON Bf ya Uholanzi na baadaye tarehe 13 Machi 2015 Kampuni ya Grewalls Saw Mills ilisaini makubaliano na MELJON Bf kwa kuuza hisa zake asilimia 20. Hivyo kampuni ya MELJON Bf iliendelea kuwa mmiliki wa kiwanda kwa asilimia 100.

Mheshimiwa Spika, kufuatia zoezi la ubinafsishaji wa viwanda, mwekezaji MELJON Bf alitakiwa kuwekeza kulingana na mkataba. Kutokana na uwekezaji huo kutofanyika, tarehe 16 Oktoba, 2018 Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina ilifanya maamuzi ya kukirejesha kiwanda na mwekezaji alipewa barua ya kuvunja mkataba.

Mheshimiwa Spika, Msajili wa Hazina anamalizia taratibu za kukirejesha kisheria kiwanda hiki Serikalini. Urejeshaji huu ukikamilika ndipo uwekezaji mpya utafanyika ili kuwezesha kukifufua kiwanda hicho. Nakushukuru sana. (Makofi)