Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 5 Sitting 5 Works, Transport and Communication Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi 53 2021-11-08

Name

Abdallah Dadi Chikota

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyamba

Primary Question

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza: -

Je, Serikali imeweka vivutio gani maalum ili kuwavutia wasafirishaji kutumia Bandari ya Mtwara kusafirisha mizigo ya nchi za Msumbiji, Malawi na Zambia?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WIZIRA YA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika hatua za awali za kuvutia wasafirishaji kutumia Bandari ya Mtwara, Serikali imepunguza asilimia 30 ya gharama za tozo za bandari kwa shehena ya Korosho. Gharama hizo zinahusisha kupanga na kupokea shehena kwenda au kutoka melini, usafiri wa kati wa kusafirisha bidhaa kutoka melini hadi kwenye eneo la kuhifadhia mizigo na kinyume chake; kupokea na kupeleka mizigo kutoka kwenye mabehewa au malori kwenda melini; na upakuaji na uhifadhi wa mizigo kutoka kwenye meli.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali imetoa punguzo la ada inayotozwa kwa matumizi ya gati kushusha mizigo ndani ya meli (wharfage) kutoka dola ya Kimarekani hadi nusu Dola na kurefusha muda wa makasha ya kupakia Korosho kuwa bure katika msimu wote wa korosho.

Mheshimiwa Spika, vile vile, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeendelea kutoa punguzo la tozo maalum kwa wasafirishaji wa makaa ya mawe na saruji ili kuifanya Bandari ya Mtwara kufanya kazi katika kipindi chote cha mwaka. Serikali itaendelea kufanya tathmini na kuchukua hatua stahiki kwa lengo la kuvutia matumizi ya Bandari ya Mtwara.

Mheshimiwa Spika, napenda kutoa wito kwa wasafirishaji kutumia punguzo hili la tozo lililofanywa na Serikali kusafirisha mizigo ya nchi za Msumbiji, Malawi na Zambia kupitia Bandari ya Mtwara. Ahsante.