Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 4 Sitting 7 Industries and Trade Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara 86 2021-09-08

Name

Assa Nelson Makanika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kaskazini

Primary Question

MHE. ASSA N. MAKANIKA aliuliza: -

Je, Serikali imefikia hatua gani katika kurekebisha vifungashio vya mafuta ya mawese kwa kuwa wananchi wanaumizwa na kunyonywa kupitia vifungashio vinavyotumika sasa?

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Assa Nelson Makanika, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo, Mkoa wa Kigoma limeshatengeneza sampuli za vifungashio vya mafuta ya mawese vitakavyotumiwa na wakulima. Kwa kuanzia SIDO imetengeneza sampuli za vifungashio hivyo vya lita tano na lita ishirini. Vifungashio hivyo viko katika mfumo wa ndoo ya chuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua inayofuata ni sampuli hizo za vifungashio kuwasilishwa kwa Wakala wa Vipimo kwa ajili ya uhakiki wa ujazo huo. Aidha, baada ya Wakala wa Vipimo kuhakiki vifungashio hivyo, itawasilisha sampuli hizo za vifungashio kwa SIDO ili viweze kuzalishwa kwa wingi kwa maana ya kibiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshatoa maagizo kwa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) na Wakala wa Vipimo kuharakisha zoezi hilo la urekebishaji wa vifungashio hivyo ili wakulima wa mawese Kigoma wasiendelee kunyonywa. Aidha, SIDO wataanza kuzalisha kwa wingi vifungashio hivyo na kuviuza kwa bei nafuu kwa wazalishaji wa mafuta ya mawese nchini ili kutekeleza kwa vitendo agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, alilolitoa wakati alipokuwa katika ziara yake Mkoani Kigoma mwezi Februari, 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.