Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 4 Sitting 7 Finance and Planning Wizara ya Fedha na Mipango 84 2021-09-08

Name

Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Primary Question

MHE. ATHUMAN A. MAIGE aliuliza: -

(a) Je, ni wakulima wangapi wadogo wadogo wamepata mikopo kutoka Benki ya Kilimo ili kukuza tija kwa wakulima hao?

(b) Je, riba za Benki ya Kilimo zinatofauti gani na riba za Benki za Biashara katika kumsaidia mkulima mdogo?

Name

Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Athuman Almas Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo: -

(a) Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Julai, 2021 Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) imekwishatoa mikopo yenye jumla ya shilingi bilioni 281.74 kwa ajili ya kuendeleza miradi ya kilimo, ufugaji na uvuvi nchini. Mikopo hiyo imewanufaisha wakulima 1,514,695 vikiwemo vyama vya wakulima 151 hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, sambamba na utoaji wa mikopo ya moja kwa moja, Benki ya Maendeleo ya Kilimo inasimamia Mfumo wa Dhamana kwa Wakulima Wadogo (Smallholder Credit Guarantee Scheme – SCGS) unaolenga kuchagiza mabenki na taasisi za fedha kuongeza ukopeshaji katika sekta ya kilimo. Hadi kufikia mwisho wa mwezi Juni 2021, SCGS ilitoa udhamini wa mikopo kwa wakulima wadogo 11,244, vikundi vya wakulima 181 na SMEs 43 waliopata mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 89.92 kutoka benki 9 washiriki katika uendeshaji wa mfuko wa SCGS.

(b) Mheshimiwa Spika, kwa upande wa riba, Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) imeweka utaratibu wa kutoza riba kwa kiwango cha asilimia 10 kwa kuzingatia uwezo wa wazalishaji wa madaraja tofauti katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi. Kwa maana hiyo, mikopo inayotolewa kwa wakulima wadogo hutozwa riba nafuu isiyozidi asilimia 10 na kwa masharti nafuu ya urejeshwaji wake yanayozingatia misimu ya mavuno na mauzo ya mazao.