Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 3 Sitting 33 Regional Administration and Local Government Authorities Ofisi ya Rais TAMISEMI. 273 2021-05-21

Name

Michael Mwita Kembaki

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Mjini

Primary Question

MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:-

Je, ni sheria ipi ambayo ilitumika kuchukua ardhi ya Mlima Nkongore kutoka kwa wananchi na kulipatia Jeshi la Magereza?

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na kwa niaba ya Waziri wa Nchi. Ofisi ya Rais -TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Kembaki Michael, Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mlima Nkongore upo katika Halmashauri ya Mji Tarime na una eneo lenye ukubwa wa ekari 266.65. Eneo hilo halina mchoro wa mipango miji na halijamilikishwa. Wananchi wanaozunguka eneo hilo walikuwa wakiutumia Mlima Nkongore kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo ukataji kuni, uchomaji mkaa na kilimo, shughuli ambazo zilikuwa zinahatarisha mazingira ya Mlima Nkongore.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi Novemba, 2017 Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tarime ilikabidhi eneo hilo kwa Jeshi la Magereza ili kuhakikisha kuwa eneo hilo linalindwa kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira Na. 20 ya mwaka 2004 kwa maana ya Environmental Management Act, 2004; kifungu cha 58(1) na (2) ambacho kinazuia kufanya shughuli zozote zinazoweza kusababisha hifadhi ya mlima kuharibiwa. Halmashauri ya Mji Tarime kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira inakamilisha taratibu za kulifanya eneo la Mlima Nkongore kuwa hifadhi. Hivyo, eneo la Mlima Nkongore litaendelea kuwa chini ya uangalizi wa Magereza hadi hapo taratibu zitakapokamilika na kulitangaza kuwa eneo hilo kuwa hifadhi.