Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 3 Sitting 28 Lands, Housing and Human Settlement Development Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi 240 2021-05-12

Name

Dunstan Luka Kitandula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkinga

Primary Question

MHE. DUNSTAN L. KITANDULA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itafuta hati ya mashamba yaliyotelekezwa kwa zaidi ya miaka 20 Wilayani Mkinga hususan shamba la Kwamtili ili ardhi hiyo igawiwe kwa wananchi?

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi (Sura 113), kila mmiliki wa ardhi anapaswa kuendeleza ardhi yake aliyomilikishwa kwa kuzingatia masharti yaliyoainishwa katika nyaraka za umiliki. Kwa wamiliki wanaobainika kukiuka masharti ya umiliki, sheria hiyo imeelekeza hatua mbalimbali za kuchukua ikiwemo kubatilisha milki husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa mashamba yenye milki za hati Na. 14501 (Ekari 2,841) na hati Na. 4722 (Ekari 58) Kwamtili, Wilayani Mkinga yanayomilikiwa na Kampuni ya Kwamtili Estate Limited kwa matumizi ya kilimo yana ukiukwaji wa masharti ya umiliki ikiwemo wamiliki kushindwa kuyaendeleza na kukwepa kulipa kodi ya ardhi kikamilifu. Hata hivyo, imebainika kuwa, katika Daftari la Kumbukumbu la Msajili wa Hati, hatimilki za mashamba hayo zimewekwa rehani kwa kukopeshwa fedha na hivyo kuwa na third part interest (maslahi ya mtu wa tatu).

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imeelekeza Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga kuanza kuchukua hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kutuma Ilani ya Ubatilisho kwa wamiliki. Hatua hiyo ikifanyika sambamba na kuwasiliana na Benki iliyotoa mkopo kama dhamana kuwataarifu wahusika kutafuta dhamana nyingine kutokana na masharti ya mashamba hayo kukiukwa. Mara baada ya milki za mashamba hayo kubatilishwa, hatua za kuyapanga, kuyapima na kuyagawa upya kulingana na mahitaji halisi sasa zitaendelea.