Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 3 Sitting 21 Information, Culture, Arts and Sports Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo 175 2021-05-03

Name

Ravia Idarus Faina

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Makunduchi

Primary Question

MHE: RAVIA IDARUS FAINA aliuliza: -

Je, Kwa nini Vyama vya Michezo ikiwemo TFF na TOC vimekuwa vikibadili Katiba zao kwa lengo la kulinda viongozi waliopo madarakani na kudhibiti watanzania wengine wasigombee nafasi katika vyama hivyo?

Name

Pauline Philipo Gekul

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa uhai siku ya leo tukaendelea kutimiza wajibu wetu sisi Wabunge wa Bunge hili. Lakini pia nimshukuru Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kuniamini tena na kunifanya Naibu katika Wizara hii. Mheshimiwa Rais nakushukuru sana. Lakini la tatu pia, niwatakie kila la kheri wanahabari wote kote nchini na duniani pia katika maadhimisho ya siku yao ya uhuru wa vyombo vya habari.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ravia Idarus Faina, Mbunge wa Makunduchi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Vyama vya Michezo Tanzania vinasajiliwa kwa Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa na 12 ya Mwaka 1967 na marekebisho yake Na. 6 Mwaka 1971 pia namba 3 ya Mwaka 2018; pamoja na kanuni za msajili za Mwaka 1999.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mahitaji ya kubadili katiba za vyama kujitokeza na kufanyika katiba hizo haziwezi kuanza kufanya kazi, mpaka zisajiliwe upya na Msajili wa Vyama vya Michezo ambaye hupitia upya, kuona kama kanuni zinazosimamia Michezo na Sheria zingine za nchi zimeangaliwa. Iwapo msajili atabaini kuwa suala ambalo limeingizwa katika katiba halina maslahi kwa Chama na Taifa ikiwemo masuala ya utawala bora; Msajili amepewa mamlaka ya kisheria kukataa usajili huo kwa mujibu wa Kanuni za Usajili za Mwaka 1999, kifungu 11(3)(a) na (b).

Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Shirikisho la TFF na TOC haijawahi kubadili katiba zao kwa lengo la kulinda viongozi walioko madarakani kwa kuwa, mabadiliko hayo yote ya kikatiba ni lazima yakidhi vigezo vya usajili vinavyosimamiwa na msajili wa vyama na vilabu vya Michezo nchini, ikiwemo utawala bora na ukomo wa muda wa uongozi chini ya BMT.