Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 3 Sitting 12 Works, Transport and Communication Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi 101 2021-04-19

Name

Deus Clement Sangu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Primary Question

MHE. DEUS C. SANGU aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya kilometa 200 kutoka Kilyamatundu kupitia Ilemba, Muze, Mfinga mpaka Majimoto?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Kwela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Kilyamatundu – Muze – Mfinga – Kasansa hadi Majimoto yenye urefu wa kilometa 206 ni barabara ya Mkoa inayosimamiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara nchini yaani TANROADS. Barabara hii inaunganisha Mkoa wa Rukwa na Mkoa wa Songwe eneo la Kilyamatundu na Kamsamba katika Daraja la Momba.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hii, Serikali ilianza kuchukua hatua za kuimarisha barabara hii kwa kuanza na kukamilisha ujenzi wa Daraja la Momba lenye urefu wa mita 84 na barabara za maingilio zenye urefu wa kilometa 1.2 ambalo lilikuwa ni kikwazo kikubwa sana cha mawasiliano baina ya Mikoa ya Rukwa, Katavi na Songwe.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Ntendo – Muze – Kilyamatundu ambao unahusisha sehemu ya Kilyamatundu – Muze yenye urefu wa kilometa 142. Kazi ya usanifu imefikia asilimia 50. Mara usanifu wa kina utakapokamilika, maandalizi ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami yataanza kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.