Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 3 Sitting 6 Lands, Housing and Human Settlement Development Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi 47 2021-04-09

Name

Eng. Stella Martin Manyanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nyasa

Primary Question

MHE. NAPE M. NNAUYE K.n.y. MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha gharama za kuhamisha umiliki wa ardhi ambazo siyo rafiki hasa kwa wanyonge na kusababisha wengi kuwa na miliki bubu?

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijajibu swali hili naomba uniruhusu nimshukuru kwanza Mwenyezi Mungu kwa fursa ambayo amenipatia kuweza kuendelea kulitumikia Taifa hili, lakini zaidi sana nimshukuru Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini tena na kutuamini Wizara yetu na kuendelea kutuweka pale ili tuendelee kuitumikia Serikali hii. Namshukuru sana kwa imani hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Engineer Stella Martin Manyanya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, uhamishaji wa milki za ardhi huzingatia Sheria ya Ardhi (Sura Na. 113), Sheria ya Usajili wa Ardhi (Sura Na. 334), Sheria ya Ushuru wa Stempu (Sura Na. 189) na Sheria ya Kodi ya Mapato (Sura Na. 332) ambayo inahusika na Kodi ya Ongezeko la Mtaji. Kwa mantiki hiyo, Wizara yangu inasimamia gharama za Ada ya Uthamini, Ada ya Upekuzi katika Daftari la Msajili, Ada ya Maombi ya Uhamisho wa Milki na Ada ya Usajili ambazo ni gharama nafuu na wananchi wa kawaida wanaweza kuzimudu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu katika nyakati tofauti imekuwa ikiboresha gharama za uhamishaji na umilikishaji wa ardhi. Kwa mfano, katika mwaka wa fedha 2018/2019 gharama za tozo za mbele yaani (premium) ilipunguzwa kutoka 7.5% kwenda 1% ya thamani ya ardhi ambayo hutozwa mara moja tu wakati wa umilikishaji kwa maeneo ya urasimishaji mijini na hadi 2.5% kwa maeneo mengine. Aidha, Wizara pia imeboresha gharama za urasimishaji kwa kupunguza kutoka shilingi 250,000/= hadi shilingi 150,000/= na katika Halmashauri nyingine wanatoza shilingi 50,000/=.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua zinazotekelezwa na Serikali zinalenga kuboresha gharama za umilikishaji na uhamishaji wa milki kuwa rafiki hususan kwa wanyonge. Aidha, kwa kuhakikisha kuwa ada na tozo zinakuwa rafiki na zinazingatia maoni ya wananchi, Serikali sikivu ya Awamu ya Tano kupitia Kamati Maalum (Task Force on Tax Reform) kila mwaka inapitia sheria za kodi ili kufanya maboresho.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, Serikali iko tayari kupokea maoni na ushauri wa wadau kuhusu viwango vya tozo zinazohusu uhamisho wa milki za ardhi na tozo nyingine zinazohusu Sekta ya Ardhi kwa ujumla ili kuboresha huduma kwa wananchi.