Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 2 Sitting 2 Energy and Minerals Wizara ya Nishati 26 2021-02-03

Name

Augustine Vuma Holle

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Vijijini

Primary Question

MHE. AUGUSTINE V. HOLLE Aliuliza: -

Je, ni lini Mkoa wa Kigoma utaunganishwa na umeme wa Gridi ya Taifa?

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Augustine Vuma Holle, Mbunge wa Kasulu Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kigoma unapata umeme kupitia mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta ya diesel ambayo ni gharama kubwa kwa TANESCO na Serikali kwa ujumla. Katika hatua ya haraka, Serikali inatekeleza mradi wa kuunganisha Mkoa wa Kigoma katika Gridi ya Taifa kutoka Tabora.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu utahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Kigoma kupitia Urambo na Nguruka umbali wa kilomita 395, pamoja na ujenzi wa vituo vya kupozea umeme wa msongo wa kilovoti 132 kwenda 33 vya Urambo, Nguruka na Kidahwe Mkoani Kigoma. Gharama za mradi huu ni shilingi bilioni 142.7 na mradi ulianza ujenzi mwezi Juni, 2020 na unatarajia kukamilika mwezi Juni, 2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hatua nyingine Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa njia kuu za kusafirisha umeme, msongo wa kilovoti 400 yenye urefu wa kilomita 280 ya kutoka Nyakanazi Mkoa Kagera hadi Kidahwe Mkoani Kigoma. Mradi huu unahusisha ujenzi wa vituo viwili vya kupoza umeme msongo wa kilovoti 400 kuja 220 kwenda 132 mpaka 33 na 400/132/33 vya Nyakanazi vyenye transfoma mbili zenye ukubwa wa MVA 120.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa mradi huu pia ulianza mwezi Januari mwaka 2020 na utakamilika mwezi Juni, 2022. Gharama ya mradi ni dola za Kimarekani milioni 187 chini ya ufadhili wa Serikali ya Tanzania, Benki ya Maendeleo ya AfDB pamoja na Benki ya Maendeleo ya Korea.