Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 2 Sitting 2 Water and Irrigation Wizara ya Maji 23 2021-02-03

Name

Dr. David Mathayo David

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Same Magharibi

Primary Question

MHE. DKT. DAVID M. DAVID Aliuliza: -

Upatikanaji wa maji katika Mji mdogo wa Same ni asilimia 34; na mradi mkubwa wa maji Same – Mwanga – Korogwe umechelewa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa: -

(a) Je, ni kitu gani kilichochelewesha mradi huo na ni hatua gani zimechukuliwa kwa watu waliohusika na ucheleweshaji huo?

(b) Je, ni lini sasa mradi utakamilika?

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mema yote ambayo amenijalia hata siku ya leo nami nimekuwa mmoja wa Wabunge katika Bunge hili Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa imani kubwa aliyoonyesha juu yangu kwa sababu Bunge la Kumi na Mbili ni Bunge ambalo hakika Wabunge wote wako imara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuwashukuru sana wanawake wa Mkoa wa Mbeya kwa kunipa imani kubwa na kuona naweza kuja kuwawakilisha na kulisukuma gurudumu la maendeleo. Nakushukuru wewe binafsi Naibu Spika kwa sababu nawe ni mpiga kura wangu halali na mwaminifu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kushukuru familia yangu, hasa mume na baba yangu mzazi pamoja na watoto wangu waliofanikisha kuwa hivi nilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mhe. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza Mradi Mkubwa wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe kwa gharama ya shilingi bilioni 262. Mradi huu unahusisha ujenzi wa miundombinu ya chanzo cha maji, ulazaji wa bomba kilomita 71, vituo vya kusukuma maji 3 na matanki 7 yenye ujazo kuanzia lita laki tatu hadi milioni tisa na ulazaji wa mabomba ya kusambaza maji kilomita 204. Katika utekelezaji mradi huu mkataba wa mwisho ulitarajiwa kukamilika Machi, 2021. Hata hivyo, kumekuwepo na kasi ya utekelezaji usiyoridhisha hadi Serikali imefikia hatua ya kusitisha mikataba na wakandarasi mwezi Desemba, 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inafanya juhudi kuhakikisha taratibu za kupata wakandarasi wapya wa kumalizia kazi za mifumo ya umeme na ulazaji wa bomba kuu kilomita 34.

Aidha, kazi za ulazaji wa mabomba ya kusambaza maji zinatekelezwa na wataalam wa ndani wa Wizara wakishirikiana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa kumtumia mkandarasi wetu Seprian Lwemeja.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatarajia mradi huu ukamilike Desemba 2021 na utanufaisha wananchi wapatao 438,820 kwa Mji wa Same-Mwanga pamoja na vijiji 38 vya Wilaya ya Same, Mwanga na Korogwe. Awamu ya kwanza itahudumia wananchi 168,820 katika miji ya Same na Mwanga. Awamu ya pili ambayo utekelezaji wake utaanza mwaka wa fedha 2021/2022 utanufaisha wananchi 270,000 katika vijiji vilivyo eneo la mradi ambapo Wilaya ya Same ni Hedaru, Mabilioni, Gavao, Makanya, Mgwasi, Bangalala, Chanjo, Mwembe, Njoro, Majengo, Bendera, Mkonga, Ijinyu na Mgandu; Wilaya ya Mwanga ni Kifaru, Kiruru Ibwejewa, Kisangara, Lembeni, Kivegere, Mbambua, Kileo, Kivulini, Kituri na Mgagao; na Wilaya ya Korogwe ni Bwiko, Mkomazi, Nanyogie, Manga-Mtindilio na Manga-Mikocheni.