Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 15 Sitting 50 Energy and Minerals Wizara ya Nishati 432 2019-06-21

Name

Susan Limbweni Kiwanga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Mlimba

Primary Question

MHE. DEVOTHA M. MINJA (K.n.y. MHE. SUSAN L. KIWANGA) aliuliza:-

Kata za Mchombe, Igima, Mbingu, Namwawala na Idete katika Jimbo la Mlimba zilipelekewa mradi wa umeme kwa gharama nafuu lakini mradi huo umefanywa vibaya na hivyo kusababisha wananchi wengi kukosa umeme:-

(a) Je, ni lini Serikali itapeleka umeme kwa wananchi hao?

(b) REA ilikabidhiwa mkandarasi kupima maeneo yatakayounganishwa umeme katika vijiji vya Msolwa, Miembeni, Iduimdembo, Ipungusa, Matema, Lumumwe, Uchindile, Kitete na Ngwasi katika Awamu ya Pili; Je, kwa nini kazi hiyo inasuasua?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mbunge wa Mlimba lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa umeme kwa gharama nafuu (Low Cost Design) katika Mkoa wa Morogoro ulitekelezwa katika vijiji 14 vya Wilaya ya Kilombero. Kazi za mradi zilihusisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 35.2; njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilomita 82.6; ufungaji wa transfoma 262 za KVA 15 na 25; pamoja na kuunganisha umeme wateja 4,671. Gharama ya mradi ni shilingi bilioni 6.935.

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia mwezi Desemba, 2018 vijiji vyote 14 vya Mkusi, Njage, Ngajengwa, Igima, Mbingu, Kisegese, Namawala, Idete Magereza, Miwangani, Katurukira, Mihelule, Mikoleko, Msolwa Station na Nyange vilipatiwa umeme na wateja 4,286 waliunganishwa na huduma ya umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mradi huo wa Low Cost Design katika Wilya ya Kilombero hususan Jimbo la Mlimba, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza inapeleka umeme katika Jimbo la Mlimba katika vijiji vya Ipugusa, Msolwa, Kalengakelu, Miembeni, Iduindembo, Ipungusa, Matema, Lumumwe, Uchindile, Kitete, Idandu na Ngwasi. Kazi zinazofanywa kwa sasa ni pamoja na kusimika nguzo, kuvuta nyaya na kufunga transfoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia utekelezaji wa mradi huu, Kijiji cha Kalengakelu kimepatiwa umeme na wateja zaidi ya 20 kutoka Vitongoji vya Usalama na Samora vimeunganishiwa umeme. Kazi ya kupeleka umeme katika vijiji hivi itakamilika mwezi Juni, 2020, ahsante sana.