Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 15 Sitting 38 Health and Social Welfare Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto 318 2019-05-29

Name

Khadija Nassir Ali

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. RASHID A. SHANGAZI (K.n.y. MHE. KHADIJA NASSIR ALI) aliuliza:-

Uzito mkubwa wa mwili ni dalili za mwanzo za magonjwa yasiyoambukiza:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kupambana na magonjwa haya?

(b) Je, mbali na mazoezi ni mbinu gani nyingine za kitaalamu za kupambana na vitambi?

Name

Ummy Ally Mwalimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Nassir Ali, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto mnamo mwaka 2011 ilianzisha rasmi kitengo cha kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa lengo maalum la kukinga na kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Aidha tumetengeneza mpango mkakati wa kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza wa mwaka 2016-2020, ambao umewekwa malengo bayana, mikakati na utekelezaji wake ili kupambana na ongezeko la magonjwa haya. Mikakati inayotekelezwa katika mkakati huu ni pamoja na utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu magonjwa haya na kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo vipeperushi, redio, runinga, mitandao ya kijamii, na nyinginezo ili kuongeza uelewa kwa jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kupunguza viashiria vya hatari ambavyo vinaweza kurekebishika kwa kuhamasisha juu ya ufanyaji wa mazoezi, ulaji unaofaa, kuhamasisha kuacha matumizi ya tumbaku na pia kupunguza unywaji wa pombe kupita kiasi. Kuhakikisha huduma za uchunguzi wa awali, yaani screening for early detection, kwa magonjwa haya zinapatikana katika vituo vya afya pamoja na fanya kambi za wazi za kupima na kutibu magonjwa haya. Kutoa chanjo kwa magonjwa yanayoweza kukingwa kwa njia hii mfano, chanjo ya HPV kwa ajili ya kujikinga na saratani ya shingo ya uzazi.

Mheshimiwa Spika, ikitokea kwa bahati mbaya, ugonjwa umegundulika katika hatua za mwisho, pia eneo hili halijasahaulika. Wizara ina mkakati ambao unashughulikia uimarishaji wa huduma za tiba shufaa yaani palliative care na pia huduma ya tiba ya utengamao yaani rehabilitation services. Upo pia mkakati unaoangalia maeneo ya tafiti ili kuimarisha suala zima la upatikanaji wa takwimu sahihi za magonjwa haya.

Mheshimiwa Spika, kitambi ni dalili mojawapo ya uzito uliopita kiasi, hii si dalili njema na hupelekea magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Njia bora ya kupambana na kitambi ni kujikinga kwa kutokukipata kwa kuhakikisha unazingatia ulaji wa vyakula unaofaa na kufanya mazoezi. Iwapo mtu akiwa ameshakipata kitambi, basi njia mojawapo ya kuondokana nacho ni kuzingatia ulaji unaofaa kwa kupunguza kiwango cha vyakula vya wanga, kupunguza kiwango cha sukari, chumvi na mafuta kwenye chakula. Kunywa maji yasiyopungua lita moja na nusu kwa siku kwa mtu mzima na kupunguza unjwaji wa pombe uliopitiliza. (Makofi)