Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 15 Sitting 37 Justice and Constitutional Affairs Katiba na Sheria 310 2019-05-28

Name

Janet Zebedayo Mbene

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ileje

Primary Question

MHE. JANET Z. MBENE aliuliza:-

Serikali iliingia Mikataba na Uwekezaji na Wadau mbalimbali kwenye Sekta tofauti ambayo kwa sababu mbalimbali imesitishwa na Serikali?

(a) Je, ni Mikataba mingapi imesitishwa na ni sekta zipi zinaongoza?

(b) Je, Serikali imeingia gharama kiasi gani, katika kesi zilizofunguliwa Mahakamani na kusitishwa kwa Mikataba hiyo?

(c) Je, Serikali imepata faida au hasara gani kwa kusitisha Mikataba hiyo?

Name

Dr. Augustine Philip Mahiga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janet Zebedayo Mbene Mbunge wa Ileje, lenye sehemu (a) (b) na (c) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Ni kweli Serikali imekuwa ikisitisha Mikataba ya Uwekezaji kutokana na sababu mbalimbali, moja ikiwa ni kwa upande mmoja mwingine ni Mkataba wa kushindwa kutimiza masharti kwa mujibu wa Mkataba au makubaliano ama inapobainika kuwa kulikuwa na udanganyifu ambao haukuweka wazi taarifa za msingi wakati wa kuingiwa katika Mikataba hiyo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali bado inaendelea na mapitio ya Mikataba yote, iliyoingiwa na Serikali ili kutambua kama vigezo na masharti kama ya Mikataba hiyo vinatimizwa ipasavyo. Mara zoezi hili, likikamilika Serikali itakuwa na takwimu sahihi ya Mikataba yote, iliyosainiwa sambasamba na kuifanya tathmini ya gharama zake zilizotumika kwa kesi zilizofunguliwa kutokana na usitishwaji wa Mikataba husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Hati Idhini ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyochapishwa katika gazeti la Serikali kwa Tangazo namba 48 la mwaka 2018 na Sheria ya marekebisho mbalimbali ya Sheria ambayo pamoja na mambo mengine imerekebisha majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambapo utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeboreshwa zaidi, kwa kuanzishwa kwa Idara itakayoishughulikia utekelezaji wa Mikataba yote baada ya kufanyiwa mapitio yaani vetting. Jukumu hili litawezesha kutambua na kupata takwimu sahihi za Mikataba yote iliyositishwa, inayotakiwa kusitishwa na inayotakiwa kufanyiwa marekebisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, Pia, mabadiliko ya Sheria hiyo yameanzisha Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ambayo kwa sasa inasimamia mashauri yote ambayo Serikali inashtaki au kushtakiwa. Kwa sasa Ofisi hii inaendelea na kazi ya utambuzi wa mashauri yote dhidi ya Serikali kutoka katika Wizara na Taasisi zote za Serikali. Jitihada zote hizi, zina malengo ya kusaidia upatikanaji wa takwimu sahihi na mashauri yaliyofunguliwa kutokana na usitishwaji wa Mikataba na kutambua faida na hasara zake.