Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 15 Sitting 23 Livestock , Fisheries, Agriculture, Food Security and Cooperatives Wizara ya Mifugo na Uvuvi 195 2019-05-08

Name

Asha Mshimba Jecha

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ASHA MSHIMBA JECHA aliuliza:-

Tanzania imebarikiwa kuwa na Ukanda wa Bahari na Maziwa.

Je, wananchi wa maeneo hayo wameandaliwaje kufaidika na rasilimali zinazopatikana katika Ukanda wa Bahari na Maziwa?

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asha Mshimba Jecha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, sekta ya uvuvi nchini inasimiwa na sera, sheria pamoja na miongozo mbalimbali iliyoandaliwa kwa lengo la kuhakikishwa wananchi na Taifa linanufaika na rasilimali za uvuvi. Pia Sera ya Uvuvi inaelekeza ushirikishwaji wa wananchi katika kusimamia rasilimali za uvuvi ambapo vimeanzishwa vikundi vya usimamizi shirikishi wa rasilimali za uvuvi kwa maana ya BMU. Vikundi hivi vinalenga kuwawezesha wananchi katika maeneo vilipoanzishwa kuwa wanufaikaji wa kwanza wa rasilimali hizi kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali ya uvuvi endelevu.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanzisha Wakala wa Mafunzo ya Uvuvi ili kuwapatia elimu vijana wa Kitanzania kuhusu masuala ya uvuvi ili nchi inufaike na rasilimali za uvuvi tulizojaliwa. Pia, Serikali imeanzisha Taasisi ya Utafiti yaani TAFIRI ili kufanya tafiti na kuvumbua teknolojia zitakazosaidia kuleta tija kwenye tasnia ya uvuvi. Taasisi hizi husaidia kuwapatia elimu na maarifa wadau wa uvuvi.

Mheshimiwa Spika, vilevile Wizara ina mikakati mbalimbali inayolenga kuleta maendeleo katika sekta ya uvuvi na kuwasaidia wavuvi ambayo ni pamoja na:-

(i) Kuendelea kutoa elimu kwa wavuvi na wadau wote kuhusu uvuvi endelevu, sera, sheria na kanuni za uvuvi ili kulinda, kusimamia, kuhifadhi na kuendeleza rasilimali za uvuvi nchini kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo;

(ii) Kuwekeza katika uvuvi wa bahari kuu kwa kufufua Shirika la Uvuvi (TAFICO), kujenga bandari ya uvuvi, kununua meli mbili kubwa za uvuvi ili kuchochea ukuaji wa viwanda vya kuchakata samaki, kuongeza thamani ya mazao, ajira na kuongeza mapato ya Serikali; na

(iii) Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wavuvi kuhusu ukuzaji wa viumbe katika maji yaani aquaculture na ufugaji samaki kwenye vizimba kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa samaki kwenye maziwa na baharini.

Mheshimiwa Spika, Wizara imeanzisha Dawati la Sekta Binafsi ili kuwasaidia wavuvi kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo kupata mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha.