Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 15 Sitting 16 Works, Transport and Communication Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano 134 2019-04-25

Name

Mahmoud Hassan Mgimwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Primary Question

MHE. MAHMOUD H. MGIMWA aliuliza:-

Barabara ya kutoka Kinyanambo A – Isalavamu – Igombavanu – Sadani hadi Madibira ilikuwepo kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2005 – 2010 na 2010 – 2015 lakini hadi sasa haijajengwa kwa kiwango cha lami:-

(a) Je, ni sababu zipi zilizofanya Serikali kutoanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami, hasa ikizingatiwa kuwa barabara hiyo ni muhimu kwa uchumi wa Wilaya za Mbarali na Mufindi?

(b) Je, ni lini sasa ujenzi wa barabara hiyo utaanza?

(c) Je, ni lini Serikali itaanza uthamini kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi wanaopisha ujenzi wa barabara hiyo?

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mahmoud Hassan Mgimwa, Mbunge wa Mufindi Kaskazini, lenye Sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Kinyanambo (Mafinga) – Madibira ni barabara ya Mkoa inayosimamiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na inajulikana kama Barabara ya Rujewa – Madibira – Kinyanambo yenye urefu wa kilometa 152. Barabara hii ambayo kwa sasa ipo katika kiwango cha changarawe, ikiunganisha Mkoa wa Iringa, sehemu ya Kinyanambo na Mkoa wa Mbeya sehemu ya Madibira, imepita maeneo muhimu yenye kilimo cha mahindi na mpunga.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) tayari imefanya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na kuandaa nyaraka za zabuni kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. Kazi hii ilikamilika mwaka 2009 ikiwa ni pamoja na kufanya uthamini kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi watakaopisha ujenzi wa barabara hiyo.

Mheshimiwa Spika, Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara hiyo kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Hata hivyo, wakati Serikali inatafuta fedha za ujenzi barabara hiyo, itaendelea kufanyiwa matengenezo mbalimbali kila mwaka ili iweze kupitika majira yote ya mwaka.