Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 15 Sitting 7 Works, Transport and Communication Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano 59 2019-04-10

Name

Abdallah Ally Mtolea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Temeke

Primary Question

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA aliuliza:-

Serikali inajitahidi kujenga barabara ili kupunguza foleni pamoja na kurahisisha usarifi na usafirishaji, lakini barabara zinawekwa matuta ambayo siyo rafiki kwa vyombo vya usafiri jambo linalosababisha baadhi ya watumiaji wa barabara hizo kuzikimbia, kwa mfano, matuta yaliyowekwa katika barabara ya Msata – Bagamoyo:-

Je, matuta ni sehemu ya alama za barabarani?

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Ally Mtolea, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, alama za barabarani hutumika kutoa ujumbe wa matumizi sahihi ya barabara katika eneo husika. Alama hizo huwekwa kwenye milingoti pembezo mwa barabara au huchorwa katika uso wa barabara kutoa tafsiri sahihi ya matumizi ya barabara. Hata hivyo, kutokana na baadhi ya madereva kutozingatia alama za barabarani hususan, alama za ukomo wa mwendo (speed limit), Serikali hulazimika kujenga matuta katika maeneo ambayo ni hatarishi ili kuwalazimisha madereva kupunguza mwendo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua kuwa baadhi ya matuta ya barabarani siyo rafiki kwa vyombo vya usafiri, Serikali iliandaa mwongozo wa usanifu wa barabara wa mwaka 2011 Road Geometric Design Manual, 2011 ambapo pamoja na mambo mengine, imeweka viwango bora vya ujenzi wa matuta barabarani. Kwa kuzingatia mwongozo huo, Wizara yangu kupitia TANROADS imepitia upya matuta yote yaliyojengwa katika barabara kuu hapa nchini na kubaini kuwa matuta 323 siyo rafiki kwa vyombo vya usafiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya uboreshaji wa matuta hayo inaendelea ambapo hadi sasa matuta 281 yemerekebishwa. Baadhi ya barabara ambazo matuta yamerekebishwa ni Kibaha - Mlandizi (6), Morogoro – Iringa (12), Mara – Simiyu (matuta 12), Igawa – Songwe (matuta matatu), Uyole – Kasumulu (matuta mawili) Mwanza – Simiyu (matuta tisa), Shelui – Nzega (matuta matano), Singida – Manyara (matuta 23), Mtukula – Bukoba (matuta saba) pamoja na maeneo mengine kwa ujumla (matuta 202).

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge na wananchi kwa ujumla kuwa matuta yote ambayo hayastahili kuwepo barabarani yataondolewa na yale ambayo hayakidhi kiwango yatajengwa upya. Aidha, natoa wito kwa madereva wote nchini kuzingatia alama za barabarani ikiwemo alama za ukomo wa mwendo (Speed limit).