Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 14 Sitting 8 Energy and Minerals Wizara ya Nishati 95 2019-02-06

Name

Hasna Sudi Katunda Mwilima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Primary Question

MHE. HASNA S. K. MWILIMA aliuliza:-

Tarafa ya Nguruka ina wakazi zaidi ya 100,000 na ndio kitovu cha biashara:-

(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kupeleka umeme wa Grid ya Taifa kutoka Usinge, Wilaya ya Kaliua?

(b) Wakazi wa Kata za Mwambao, Sunuka, Kaliya, Buhigu, Igalula, Haramba na Sigunga hawana umeme na Jiografia ya kuwaunganishia umeme kutoka Uvinza ni ngumu. Je, Serikali haioni umuhimu wa kupeleka umeme kutoka Mpanda, Mwese kwenda Kata ya Kaliye, ili iwe rahisi kuzipitia kata zingine?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hasna Sudi Katunda Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini, lenye Sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza kutekeleza mradi wa kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti 400 katika Mikoa ya Kusini Magharibi, ikiwemo Mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma kwa lengo la kuwaunganisha wananchi wa maeneo hayo na Gridi ya Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hatua za awali Serikali kupitia TANESCO kwa kushirikiana na Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika imeanza kutekeleza mradi wa njia ya kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti 400 North West Grid Kv 400, Iringa – Mbeya – Tunduma – Sumbawanga
– Mpanda – Kigoma – Nyakanazi wenye urefu wa kilometa 1,372. Kwa sasa Benki ya Dunia imeshatoa dola za Kimarekani milioni 455 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na utekelezaji wa mradi huu Serikali kupitia TANESCO mwezi Disemba, 2018 imeanza kutekeleza mradi wa kuunganisha Mkoa wa Kigoma na Grid ya Taifa kutoka Mkoa wa Tabora. Mradi unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 132 kutoka Tabora, Urambo, Usinge – Kaliua, Nguruka hadi Kidahwe Kigoma Mjini wenye urefu wa kilometa 370. Kazi za mradi zinahusisha ujenzi wa vituo vya kupoza umeme vya 132/33 Kv katika Miji ya Urambo na Nguruka. Gharama ya kazi hiyo inakadiriwa kufikia dola za kimarekani milioni 81 na ujenzi wa mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Februari, 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, kukamilika kwa mradi huu na miradi mingine inayoendelea kutaimarisha upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Kigoma ikiwa ni pamoja na kuwasambazia wananchi umeme katika Kata za Mwambao, Sunuka, Kaliya, Buhigu, Igalula, Haramba na Sigunga. Nakushukuru.