Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 14 Sitting 8 Works, Transport and Communication Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano 88 2019-02-06

Name

Lucia Ursula Michael Mlowe

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. LUCIA M. MLOWE aliuliza:-

Uwanja wa Ndege wa Njombe umekuwa kero kwa wananchi, kwani upo katikati ya Mji na haujakarabatiwa kwa muda mrefu matokeo yake uwanja huo umejaa barabara hizo. Aidha, watu wanaopita katika barabara hizo zisizo rasmi hukamatwa na kutozwa faini:-

Je, ni lini mkakati wa Serikali juu ya uwanja huo ili kupunguza kero kwa wananchi hao?

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI, UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucia Michael Mlowe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanja cha ndege cha Njombe kilijengwa na Wakoloni, yaani kabla ya uhuru miaka ya 1940 na kuanza kutumika rasmi 1945. Miaka hiyo Mji wa Njombe ulikuwa mdogo sana na hivyo kiwanja kilikuwa mbali na makazi ya watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria za Kitamaifa za Usalama wa Anga hairuhusiwi watu, wanyama, magari na kadhalika kukatiza kwenye viwanja vyovyote vya ndege. Kwa mantiki hiyo, vitendo vya baadhi ya wananchi wa maeneo hayo kukatiza katika kiwanja hicho ni vya uvunjivu wa sheria na ndiyo maana wananchi hao hukamatwa na kutozwa faini au kuadhibiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika juhudi za kukarabati kiwanja cha ndege cha Njombe, Serikali imepanga kufanya upembuzi yanikifu na usanifu wa kina kwa kutumia fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia uliohusisha pia viwanja vya ndege vya Iringa, Songea, Lindi, Kilwa Masoko, Tanga, Moshi, Lake Manyara, Singida, Musoma na kiwanja kipya cha Mkoa wa Simiyu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina imekamilika kwa viwanja hivyo ambapo taarifa ya mwisho iliwasilishwa tarehe 28 Machi, 2017. Hatua iliyopo kwa sasa ni utafutaji wa fedha kutoka vyanzo mbalimbali kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa kiwanja hicho. Upanuzi huo utahusisha ujenzi wa uzio kuzunguka eneo lote la kiwanja ili kudhibiti wananchi wanaokatisha kiwanja hicho kinyume cha taratibu.