Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 11 Sitting 60 Regional Administration and Local Government Authorities Ofisi ya Rais TAMISEMI. 505 2018-06-28

Name

Issaay Zacharia Paulo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Primary Question

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Hali ya barabara zinazosimamiwa na halmashauri ni mbaya sana kutokana na fedha zinazotolewa na Mfuko wa Barabara kukaa kwa muda mrefu na hali ya kuongezeka kwa magari binafsi na yale ya biashara ambapo kila tarafa ina zaidi ya magari 20 na hivyo, kufanya barabara hizo kuharibika na kuwa vigumu kupitika nyakati za masika:-
(a) Je, Serikali haioni haja ya kuleta mapendekezo mapya ya mgao wa fedha za barabara?
(b) Barabara nyingi za Halmashauri ya Mji wa Mbulu zimejifunga katika Tarafa za Nambis na Daudi. Je, kwa nini wataalam kutoka Wizarani wasifike kuzikagua na kutoa ushauri stahili?
(c) Je, kwa nini BQ za tenda za barabara ngazi ya mkoa zisiwekwe kwenye kitabu cha RRB, ili Waheshimiwa Wabunge na wananchi wafahamu shughuli zitakazofanywa na makandarasi waliopewa kazi?

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paul Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, lenye Sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kufanya tathmini ya mtandao wa barabara nchi nzima ili hatimaye utumike kuangalia kwa kina utaratibu mzuri zaidi wa mgawo wa fedha za barabara kati ya TANROADS inayoshughulikia barabara kuu na barabara za mikoa na TARURA inayoshughulikia barabara za Mamlaka za Serikali za Mitaa.
b) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mwaka wa Fedha 2017/2018 Barabara za Mji wa Mbulu zilitengewa shilingi milioni 814.56. Kati ya hizo shilingi milioni 262.12 zilitengwa kwa ajili ya barabara kwa ajili ya matengenezo ya muda maalum (Periodic Maintenance) Barabara za Ayamaame – Kainam – Hhasama – Mbulu – Endagikot – Tlawi, Tango FDC, Waama – Masieda, Ayayumba – Hhayloto zenye urefu wa kilometa 35.7 katika Tarafa za Daudi na Nambisi na kuweka changarawe katika Barabara za Ayamaami – Kainam – Hhasama, Mbulu – Kuta na Ayayumba - Hhayloto zenye urefu wa kilometa 8.13
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuchonga barabara ya Uhama – Masieda – Hayayumba – Hailoto zenye urefu wa kilometa 31.5 na ujenzi wa kalavati za njia mbili zenye kipenyo cha milimita 900 katika Tarafa ya Daudi. Barabara zilizokuwa zimejifunga kwa kuharibika na mvua sasa zinapitika ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 95 na kazi inaendelea. Katika Mwaka wa Fedha 2018/2019 Barabara za tarafa za Nambis na Daudi zimetengewa shilingi milioni 438.8 kwa ajili ya matengenezo.
c) Mheshimiwa Mwenyekiti, ni haki ya wajumbe wa Bodi ya Barabara ya Mkoa na wananchi kupata taarifa za jumla za barabara zilizopangwa kujengwa katika mkoa, ikiwemo gharama za kazi ambazo wajumbe wanaweza kuzipata katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara ya Mkoa.