Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 11 Sitting 57 Works, Transport and Communication Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano 482 2018-06-25

Name

Jasson Samson Rweikiza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Vijijini

Primary Question

MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-
Barabara ya kuanzia Kanazi, Kata ya Kemondo kupitia Ibwera kwenda Katoro, Rubale na Izimbya ipo chini ya TANROADS, na ni muhimu kwa wakazi wa Bukoba na kwa uchumi wa Taifa:-
Je, ni lini barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami?

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara tajwa inaitwa Kyetema – Kanazi – Kyaka 2 yenye urefu wa kilometa 42.37 na inapita katika vijiji vya Ibwera na Katoro. Barabara nyingine ni Rutenge – Rubale – Kishoju yenye urefu wa kilometa 74 ambayo inapita katika Vijiji vya Izimbya na Rubale. Barabara zote hizo ni barabara za Mkoa na zinahudumiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS). Barabara hizi ni kiunganishi muhimu cha barabara kuu za lami ambazo ni barabara ya Mutukula – Bukoba – Kagoma – Lusahunga na barabara ya Kyaka – Bugene.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa baraba hizi, Serikali imekuwa ikitenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kuzifanyia matengenezo ya aina mbalimbali ili ziweze kupitika wakati wote wa mwaka. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, barabara ya Kyetema – Kanazi – Kyaka 2 imetengewa shilingi milioni 598.13 na barabara ya Rutenge – Rubale – Kishoju imetengewa shilingi milioni 333.20. Aidha, Serikali imejenga kwa kiwango cha lami maeneo korofi yenye urefu wa kilometa 4.8 sehemu ya Kyetema hadi hadi Kanazi kwenye barabara ya Kyetema – Kanazi – Kyaka 2.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa kipaumbele cha Serikali ni ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara za kuunganisha makao makuu ya mikoa, pamoja na barabara za kuunganisha Tanzania na nchi jirani. Hivyo, ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara za mikoa zikiwemo barabara za Kyetema – Kanazi – Kyaka 2 na Rutenge – Rubale – Kishoju utaendelea kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.