Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 11 Sitting 53 Enviroment Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira 448 2018-06-19

Name

Mwantum Dau Haji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MWATUM DAU HAJI aliuliza:-
Kilimo cha Tanzania hutegemea mvua za msimu ambazo kwa kiasi kikubwa zimeathiriwa na mabadiliko ya tabianchi na hivyo kuathiri shughuli za uzalishaji.
Je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi?

Name

Kangi Alphaxard Lugola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwibara

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira), napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwatum Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika Sekta ya Kilimo, Ofisi ya Makamu wa Rais iliandaa Mpango wa Taifa wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2007 na Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2012 katika sekta mbalimbali ikiwemo na sekta ya kilimo. Mipango hii kwa sekta ya kilimo imejikita katika kuendeleza kilimo cha umwagiliaji ikiwa ni pamoja na kutumia teknolojia zinazopunguza upotevu wa maji ili kuepuka kilimo cha kutegemea mvua.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, mipango hii inaelezea namna ya kubadili vipindi vya upandaji mazao ya misimu ili kuendana na mabadiliko ya misimu ikiwa ni pamoja na kupanda mazao na mbegu zinazohimili ukame, kuboresha mbinu za kudhibiti wadudu waharibifu wa mazao na kuweka mifumo mbadala ya kilimo ili kuongeza uzalishaji. Aidha, Ofisi ya Makamu wa Rais ipo katika mchakato wa kukamilisha kuandaa mpango endelevu wa Kitaifa wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (National Adaptation Plans). Mpango huu utakapokamilika utawezesha nchi kuwa na mipango itakayowezesha kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika sekta muhimu ikiwemo sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa inashirikiana na Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Maji na Umwagiliaji katika kuandaa mipango ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika Sekta ya Kilimo. Mipango iliyoandaliwa ni pamoja na:-
Moja, Mpango Mahususi wa Sekta ya Kilimo katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (Tanzania Agriculture Climate Resilience Plan); pili, Mpango wa Kitaifa wa Kilimo Rafiki cha Mabadiliko ya Tabianchi (National Climate Smart Agriculture) na programu mbalimbali za uendelezaji wa kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika utekelezaji wa mipango na programu hizi katika sekta ya kilimo, suala la kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika kilimo imezingatiwa hasa kwa kusisitiza uwekezaji katika miundombinu ya kilimo (suala la kuongeza kilimo cha umwagiliaji).