Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 11 Sitting 52 Water and Irrigation Maji na Umwagiliaji 445 2018-06-18

Name

Stephen Hillary Ngonyani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Vijijini

Primary Question

MHE. MARY P. CHATANDA - (K.n.y MHE. STEPHEN H. NGONYANI) aliuliza:-
Serikali ilitenga shilingi bilioni 13 kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Mkomazi lakini baadaye Serikali ilihamishia fedha hizo mkoa mwingine:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kurudisha fedha hizo ili bwawa lililokusudiwa lijengwe?

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba nimpe pole Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wake wa Korogwe Vijijini kwa msiba wa kufiwa na mke wake kipenzi. Mwenyezi Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu.
Mheshimiwa Spika, lakini kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stephen Hillary Ngonyani Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kati ya mwaka 2003 na 2004 wananchi wa Kijiji cha Manga Mikocheni, Kata ya Mkomazi, Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe walionesha hitaji la mradi wa kuendeleza kilimo cha umwagiliaji kwa zao la mpunga katika Bonde la Mkomazi. Aidha, kwa mwaka wa fedha wa 2006/2007, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa wakati huo kupitia Ofisi ya Umwagiliaji Kanda ya Kilimanjaro ilifanya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali ambapo walibaini kuwa jumla ya shilingi bilioni 13 zingehitajika kuendeleza bonde la Mkomazi ikiwemo ujenzi wa bwawa hilo.
Mheshimiwa Spika, aidha, upembuzi huo, ulibainisha kuwa ujenzi wa bwawa hili ungesababisha Ziwa Manga lilipopo katika Kijiji cha Manga ambalo lina maji ya chumvi kuchanganya maji yake ya Bwawa la Mkomazi hivyo maji yote kuwa ya chumvi ambayo yangeathiri kilimo cha zao la mpunga.
Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto hii mwaka 2014/2015, Ofisi ya Umwagiliaji Kanda ya Kilimanjaro ilifanya mapitio ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kuepuka kuzamisha Ziwa Manga na kubaini kuwa jumla ya shilingi bilioni 1.5 zingehitajika kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo.
Mheshimiwa Spika, katika kufikia azma hiyo, Serikali kupitia bajeti ya mwaka 2015/2016, ilitenga jumla ya shilingi milioni 800 kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Mkomazi. Hata hivyo, fedha za ndani zilizotengwa kwa ajili ya mradi huo hazikupatikana na hivyo kusababisha mradi huo kutotekelezwa.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa mradi huo na hasa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inatarajia kuliingiza bwawa hilo katika vipaumbele vya kutekeleza Mpango Kabambe wa Umwagiliaji wa Taifa ambao kwa sasa unafanyiwa mapitio kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA). Mapitio hayo yanatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2018. (Makofi)