Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 11 Sitting 49 Works, Transport and Communication Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano 422 2018-06-12

Name

Omary Tebweta Mgumba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini Mashariki

Primary Question

MHE. OMARY T. MGUMBA aliuliza:-
Barabara ya Ubena, Ngerengere hadi Mvuha ina urefu wa zaidi ya kilometa 70 na inaunganisha Wilaya ya Bagamoyo na Halmashauri ya Morogoro ambako Makao Makuu ya Wilaya mpya ya Mvuha yanatarajiwa kujengwa. Aidha, barabara hii inaunganisha Mkoa wa Pwani na Morogoro. Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro haina uwezo wa kuhudumia barabara hiyo:-
(a) Je, ni lini Serikali itakubali ombi la kupandisha barabara hiyo kuwa ya Mkoa?
(b) Je, ni lini Serikali itatengeneza barabara hiyo ya Ubena – Mvuha kwa kiwango cha changarawe ili ipitike mwaka mzima?

Name

Eng. Atashasta Justus Nditiye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omary Tebweta Mgumba, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Ubena Zomozi kwenda Ngerengere hadi Mvuha yenye urefu wa kilomita 105.4 ilipandishwa hadhi na Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano tangu Januari, mwaka 2017 kutoka barabara ya Wilaya na kuwa barabara ya Mkoa baada ya kukidhi vigezo vya Sheria ya Barabara ya mwaka 2007 na Kanuni zake za mwaka 2009. Kwa sasa barabara hii inahudumiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu kubwa ya barabara hii inapitika kwa shida hasa wakati wa masika hususani kati ya kipande cha Ngerengere na Mvuha ambacho kina urefu wa kilomita 95.4. Sehemu iliyobaki kati ya Ubena Zomozi na Ngerengere inapitika vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Morogoro, inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali katika maeneo korofi ili iweze kupitika majira yote ya mwaka. Aidha, kutokana na umuhimu wa barabara hii ya Ubena Zomozi – Ngerengere – Mvuha – Kisaki – Stiegler’s Gorge inayoelekea katika mradi wa kufua umeme kwa kutumia maporomoko ya Mto Rufiji katika mwaka wa fedha 2018/2019 wizara yangu imetenga jumla ya shilingi bilioni tano kwa ajili ya ukarabati mkubwa.