Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 12 Sitting 1 Livestock , Fisheries, Agriculture, Food Security and Cooperatives Wizara ya Mifugo na Uvuvi 08 2018-09-04

Name

Zaynab Matitu Vulu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ZAYNAB M. VULU aliuliza:-
Kilimo cha mwani kinalimwa baharini na asilimia kubwa ya wakulima wa zao hilo ni wanawake:-
(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha zao hilo?
(b) Je, Serikali inamsaidiaje mkulima wa mwani kupata soko la uhakika hususani nje ya nchi?

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaynab Matitu Vulu, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, kilimo cha zao la mwani kinachofanyika katika mwambao wa Bahari ya Hindi ni miongoni mwa shughuli za sekta ndogo ya ukuzaji wa viumbe kwenye maji ambapo jumla ya tani 1,197 zenye thamani ya shilingi milioni 412 zilivunwa na kusafirishwa nje ya nchi mwaka 2016/2017. Aidha, tani 1,329 zenye thamani ya shilingi milioni 469 zilivunwa mwaka 2017/2018. Mwani hulimwa zaidi na wanawake wanaokadiriwa kuwa asilimia 90 ya wakulima.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2005 Serikali iliandaa Mpango Madhubuti wa Maendeleo ya Mwani kwa lengo la kukabiliana na changamoto za kilimo cha mwani zikiwemo kiasi kidogo cha mwani kinachozwalishwa na wakulima pamoja na mapato duni. Malengo mahsusi ya Mpango Madhubuti wa Maendeleo ya Mwani ni pamoja na kujenga uwezo wa wakulima kujitegemea; kuongeza mwamko juu ya kilimo cha mwani kama shughuli inayozalisha mapato mazuri; na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ambayo yanachochea uwekezaji wa kisasa na kudumisha matumaini ya wadau wote wa tasnia ya mwani.
(b) Mheshimiwa Spika, mwani unaozalishwa nchini unauzwa katika masoko ya nchi za Ufilipino, Uchina, Ufaransa na Denmark. Pia kiasi kidogo cha mwani husindikwa hapa nchini na wadau kwa kutengeneza sabuni za mche, sabuni za maji na shampoo. Pia, mwani husindikwa ajili ya chakula na dawa.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaongeza kasi ya utekelezaji wa Mpango Madhubuti wa Maendeleo ya Mwani ikiwa ni pamoja na kuongeza uzalishaji; kusaidia wananchi kuingia mikataba yenye tija na makampuni ya mwani; pamoja na kutafuta masoko mapya ya nje ili kusaidia wakulima kupata bei bora zaidi.