Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 12 Sitting 1 Livestock , Fisheries, Agriculture, Food Security and Cooperatives Wizara ya Mifugo na Uvuvi 07 2018-09-04

Name

Neema William Mgaya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Halmashauri ya Makete ni miongoni mwa Halmashauri zinazozalisha maziwa ya ng’ombe kwa wingi:-
Je, ni lini Serikali itajenga Kiwanda cha Kusindika Maziwa katika shamba la Ng’ombe la Kitulo Makete - Njombe?

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Shamba la Mifugo la Kitulo linalomilikiwa na Serikali lipo Wilaya ya Makete, Mkoa wa Njombe na lina mifugo kwa maana ya ng’ombe wa kisasa wapatao 799. Ng’ombe walioko Kitulo utumika kuzalisha mitamba pamoja na maziwa.
Mheshimiwa Spika, Wizara ina mpango wa kuboresha Shamba la Mifugo la Kitulo kwa kuboresha kosaafu za ng’ombe kwa kununua ng’ombe bora wa maziwa aina ya Holstein Friesian majike 400; kuongeza ng’ombe bora wa maziwa kutoka 450 waliopo hadi kufikia ng’ombe bora wa maziwa 1,200; kuongeza uzalishaji mitamba ya kuuza kutoka mitamba 80 kwa mwaka hadi mitamba 213 kwa mwaka; na kuongeza uzalishaji wa maziwa kutoka lita 400,000 kwa mwaka hadi lita 3,350,816 kwa mwaka ifikapo mwaka 2023.
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Njombe una Kiwanda cha Kusindika Maziwa cha Njombe Milk Factory, wakati Mkoa wa jirani wa Iringa una viwanda vya ASAS Dairy na Mafinga Milk Group ambapo kwa pamoja viwanda hivi vina uwezo wa kusindika lita 56,600 za maziwa kwa siku lakini vinasindika lita 18,300 tu kwa siku. Hivyo, wananchi wa mikoa hii wanayo fursa kubwa ya kuongeza uzalishaji wa maziwa ili kuwezesha viwanda hivyo kusindika kulingana na uwezo wa viwanda hivi.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya uanzishwaji wa viwanda ikiwemo kuboresha miundombinu ya barabara; kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika; kuondoa kodi kwenye mitambo na vifaa vya kupoozesha na kusafirishia maziwa; pamoja na kuhamasisha viwanda hivi kununua magari maalum ya kusafirisha maziwa ili viweze kufikia wafugaji katika maeneo yao.