Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 11 Sitting 28 Water and Irrigation Maji na Umwagiliaji 236 2018-05-14

Name

Lucy Simon Magereli

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MWITA M. WAITARA (K.n.y. MHE. LUCY S. MAGERELI) aliuliza:-
Mradi wa Maji wa Kimbiji na Mpera chini ya Kampuni ya Serengeti Limited ulianza Machi, 2013 na Desemba 2016 ulitarajiwa kukamilisha visima 20 ambavyo vitawahudumia wananchi wa Kigamboni na Mkuranga. Waziri wa Maji na Umwagiliaji Oktoba, 2016 akitembelea mradi huo na kuagiza ukamilike kwa wakati uliopangwa vinginevyo kampuni ingelipa gharama za ucheleweshaji lakini hadi leo mradi huo haujakamilika:-
(a) Je, Serikali imeshawajibisha kampuni hiyo kwa kuchelewesha utekelezaji wa mradi huo?
(b) Je, ni lini mradi huo utakamilika ili kuondoa adha kwa wananchi wa Kigamboni ambao wengi wao wanatumia maji ya visima vifupi ambavyo sio salama?

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako kabla sijamjibu ndugu yangu, naomba nitoe shukrani za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kusikia kilio cha Waheshimiwa Wabunge kuhusu suala zima la utekelezaji wa miradi vijijini na ameagiza Wahandisi wote waje katika Wizara ya Maji. Nataka niwaambie Wahandisi wa Maji wanyooke na asiyekubali kunyooka basi tupo tayari kumnyoosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Simon Magereli, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mradi wa Uchimbaji wa Visima vya Maji vya Kimbiji na Mpera umechelewa kutekelezwa. Serikali imechukua hatua za kimkataba dhidi ya kampuni husika ikiwa ni pamoja na kukata malipo kwa ucheleweshaji wa kazi (liquidated damage). Mradi wa visima vya Kimbiji na Mpera ilikuwa ukamilike Mei, 2018 sasa unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, maji ya visima hivyo yataanza kutumika baada ya kukamilika kwa awamu ya pili ambayo itahusu ujenzi wa miundombinu ya kusambaza maji ambao utaanza kutekelezwa katika bajeti ya mwaka 2018/2019. Kwa sasa ili kuondoa adha ya wananchi wa Kigamboni wakati wanasubiri kukamilika kwa mradi mkubwa wa Kimbiji na Mpera, Serikali imeanza kutekeleza miradi mbalimbali minne ya uboreshaji wa huduma ya maji kwa mpango wa muda mfupi kwa wakazi wa Kigamboni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hiyo ni pamoja na:-
• Ujenzi wa mtandao wa mabomba ya kusambaza maji kutoka Ruvu Chini kupitia bomba linalovuka bahari eneo la Kurasini kwenda Kigamboni ili kusambaza maeneo ya Tipper, Chuo cha Mwalimu Nyerere na Kigamboni Ferry kuelekea Mjimwema;
• Mradi wa kuendeleza kisima cha Gezaulole ambacho maji yake yatasambazwa Gezaulole na maeneo ya jirani kuelekea Mjimwema;
• Mradi wa ujenzi wa miundombinu ya kusambaza maji kutoka visima vya Vijibweni kuelekea maeneo ya ofisi mpya ya Manispaa ya Kigamboni; na
• Kuendeleza kisima kirefu cha mita 600 cha Kisarawe II ili kufikisha maji Kibada na maeneo ya viwanda (light industry zone) la Kimbiji. (Makofi)