Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 11 Sitting 18 Livestock , Fisheries, Agriculture, Food Security and Cooperatives Wizara ya Mifugo na Uvuvi 150 2018-04-27

Name

Hamida Mohamedi Abdallah

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza:-
Mwaka 1974 Tanzania iliridhia Mkataba wa Kuzuia Uchafuzi wa Bahari na Usalama wa Bahari ambao lengo mojawapo ni kuzuia uvuvi haramu wa kutumia mabomu na kutoa misaada ya vifaa vya kuzuia uchafuzi wa bahari:-
(a) Je, Serikali imeweka mikakati gani ya kuzuia uvuvi haramu wa kutumia mabomu ambao bado unaendelea?
(b) Je, Serikali inawasaidiaje wavuvi ili waachane na uvuvi haramu wa kutumia mabomu?

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mikakati mbalimbali ya kupambana na uvuvi haramu ukiwemo uvuvi wa kutumia mabomu, mikakati hiyo ni pamoja na:-
(a) Kuimarisha ushirikishwaji wa jamii katika kusimamia na kulinda rasilimali za uvuvi kupitia Halmashauri, Serikali za Vijiji na Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi kwa maana ya BMUs;

(b) Kuendelea kutoa elimu kuhusu athari za uvuvi haramu kwa mazingira, jamii na uchumi;
(c) Kufanya maboresho ya sheria ili kuwa na sheria kali dhidi ya uvuvi haramu hasa uvuvi wa kutumia mabomu ama milipuko ikiwa ni pamoja na kuweka kipengele cha kuonesha uvuvi haramu ni uhujumu wa uchumi; na
(d) Kuimarisha Mashirikiano ya Kikanda na Kimataifa kwa kushirikiana na nchi mbalimbali zikiwemo nchi za SADC katika kuzuia uvuvi usioratibiwa na usioripotiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inaendelea kufanya operesheni ikiwa ni pamoja na Operesheni Sangara, Jodari na operesheni za Kikosi cha Kitaifa kwa maana ya Mult Agency Task Team (Matt) cha kuzuia uharibifu wa mazingira ili kulinda rasilimali za uvuvi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia MATT, Serikali imefanya operesheni katika Mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Tanga na Dar es Salaam ambapo mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kupungua kwa idadi ya milipuko kutoka asilimia 88 kwa mwezi hadi kufikia asilimia mbili mwezi Machi 2018, kukamatwa kwa vifaa vya milipuko na watuhumiwa 32 ambapo kesi 13 zimefunguliwa mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuwasaidia wavuvi kuachana na uvuvi haramu ukiwemo wa kutumia mabomu, Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wavuvi wa jamii za Ukanda wa Pwani kuhusu athari za uvuvi haramu kama vile uharibifu wa mazingira, matumbawe, mazalia na makulio ya samaki, kusababisha jangwa katika bahari, kuua viumbe vingine visivyo kusudiwa, vifo, ulemavu ili waache kabisa vitendo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali inaendelea kuwahimiza wavuvi kujiunga katika vikundi na kuanzisha Vyama vya Ushirika vya Msingi, Vyama vya Akiba kwa maana ya SACCOS na VICOBA ili waweze kukopesheka na kuweza kununua zana na vyombo bora vya uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye injini za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu pamoja na nyuzi kwa ajili ya nyavu za uvuvi na vifungashio kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2011na Sheria ya Mamlaka ya Mapato (VAT) ili kuwasaidia wavuvi kupata zana za uvuvi kwa bei nafuu. Aidha, Serikali inahamasisha sekta binafsi kujenga viwanda vya kutengeza boti na zana bora za uvuvi ili kuwezesha wavuvi kuzipata kwa bei nafuu na kwa urahisi.