Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 11 Sitting 11 Industries and Trade Viwanda na Biashara 88 2018-04-17

Name

Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-
Wananchi wengi wa Tarafa ya Eyasi katika Wilaya ya Karatu wanajishughulisha na kilimo cha vitunguu maji, hata hivyo mavuno yanayotokana na kilimo hicho hupimwa kwa debe yanapouzwa badala ya kilo.
Je, ni kwa nini Serikali isihakikishe na kusimamia uuzwaji wa mazao haya kwa kutumia kilo badala ya vipimo vya debe?

Name

Jenista Joackim Mhagama

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Peramiho

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Namba 340 ya mwaka 2002 na mapitio yake ya mwaka 2016, vipimo sahihi ni kutumia mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo na siyo vinginevyo ambapo kipimo chake ni kilo kwa bidhaa za aina hii yaani vitunguu vikiwa ni mojawapo vinavyostahili kupimwa kwa kilo.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Wakala wa Vipimo inaendelea kutoa elimu kwa umma juu ya matumizi sahihi ya vipimo kwa njia ya redio, luninga, makala za magazeti na kwa kushiriki katika maonesho mbalimbali. Vilevile Wakala wa Vipimo wametoa elimu kwa wadau wa biashara hiyo ya vitunguu huko Mang’ola Tarafa ya Eyasi wakiwemo wakulima, viongozi wa vijiji, kata, tarafa, halmashauri ya wilaya kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu matumizi sahihi ya vipimo vinavyoruhusiwa kisheria.
Mheshimiwa Spika, ili kurahisisha utekelezaji wa Sheria ya Vipimo ilipitiwa na Bunge lako Tukufu mwezi Novemba, 2016 ili kuruhusu Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwa na Sheria Ndogo (by-laws) za kuwawezesha kuanzisha vituo vya ununuzi wa mazao na bidhaa katika eneo la mamlaka husika vitakavyokuwa na mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo. Hali kadhalika, Serikali inaendelea kuhamasisha ujenzi wa vituo maalum vya ununuzi wa mazao (buying centres) vyenye nafasi ya maghala ya kuhifadhia mazao, ambapo kwa Tarafa ya Eyasi, Halmashauri ya Wilaya ya Karatu kwa kushirikina na wadau wa maendeleo tayari imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa kituo katika kijiji cha Mang’ola chenye maghala matatu kwa ajili ya kuhifadhi vitunguu. Kituo hiki kinatarajia kuanza kutumika katika msimu wa mwaka huu wa ununuzi wa vitunguu. Vituo vya aina hii vitasaidia wakulima kuwa na nguvu ya pamoja kujadiliana na wanunuzi na kutumia vipimo sahihi ili kupata bei yenye ushindani na haki katika soko.
Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge lako Tukufu ninapenda kuwatahadharisha wakulima na wafanyabiashara wote wanaojihusisha na biashara ya vitunguu na mazao mengine yote kuhakikisha kuwa wanatumia vipimo sahihi. Aidha, Serikali itaendelea kufuatilia kuchukua hatua za kisheria pale inapobidi kufanya hivyo kwa wanaokiuka sheria hiyo.