Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 3 Sitting 8 Natural Resources and Tourism Wizara ya Maliasili na Utalii 71 2016-04-29

Name

Kiswaga Boniventura Destery

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magu

Primary Question

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA aliuliza:-
Serikali ilitenga eneo la Sayaka Salama Bugatu kuwa hifadhi ya msitu, lakini msitu wenyewe haukui huku wananchi, wafugaji na wakulima wakikosa maeneo ya mifugo yao na kilimo.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwarudishia wananchi maeneo hayo ili waweze kuyatumia kwa kilimo na mifugo.

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniventura Desdery Kiswaga, Mbunge wa Magu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, msitu na hifadhi Sayaka ulitangazwa rasmi kuwa Msitu wa Hifadhi chini ya Serikali Kuu kwa Tangazo la Serikali namba 90 la tarehe 19 Juni 1996. Katika siku za nyuma Halmashauri ya Wilaya ya Magu iliomba kubadilishwa kwa matumizi ya msitu huu wenye ukubwa wa hekta 5421, lakini kwa kuzingatia sababu za msingi za kiuhifadhi, Wizara kupitia barua kumbukumbu namba JA/66/298/02/33 ya tarehe 19 Desemba, 2001 ilikataa ombi hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hifadhi ya msitu wa Sayaka ni sehemu muhimu sana inayochuja na kudhibiti taka nyingi kutoka mto Duma unaopita katika hifadhi hii. Uwezo huu wa kudhibiti na kuchuja taka ambazo ni pamoja na tope na viuatilifu vinavyotoka mashambani unatokana na uoto wa asili uliopo ambao unahitaji kuboreshwa zaidi ili uendelee kupunguza athari za tope na viuatilifu katika Ziwa Victoria.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, hatua ya kubadilisha msitu huu na kuwa mashamba eneo la kuchungia mifugo au shughuli nyingine za kibinadamu zisizo za uhifadhi itasababisha kupotea kwa uoto wa asili na kusababisha mmomonyoko mkubwa wa udongo ndani ya hifadhi na hivyo kuruhusu taka nyingi kuingia ziwani jambo ambalo litapunguza uhifadhi wa mazingira ya Ziwa Victoria ambalo ni muhimu kwa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu mkubwa wa msitu wa Sayaka, Serikali haina mpango wa kubadilisha matumizi yake kinyume na malengo ya kuanzishwa kwake, kwani hatua hiyo itasababisha athari kubwa na nyingi za kimazingira na kiuchumi. Aidha, wananchi wanaoishi vijiji vinavyozunguka Msitu wa Hifadhi ya Sayaka ndiyo watakaokuwa waathirika wa kwanza kwa upepo mkali, upungufu wa mvua utakaoathiri mifugo na kilimo na athari nyinginezo kwa siku zijazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuanzishwa kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania mnamo mwaka 2011, usimamizi na ulinzi wa misitu huu umeimarishwa na kufanya uoto wa asili kurejea kwa kufanya marejeo ya soroveya, kuimarisha mipaka na kuweka vigingi 65 katika mipaka. Aidha, Kamati za Maliasili za Vijiji Kumi ndani ya Halmashauri ya Magu zimeanzishwa kwa ajili ya kushirikiana na wataalam katika ulinzi wa msitu huu.