Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 11 Sitting 4 Works, Transport and Communication Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano 32 2018-04-06

Name

Justin Joseph Monko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Kaskazini

Primary Question

MHE. JUSTIN J. MONKO aliuliza:-
Barabara ya Singida - Ilongero - Mintiko hadi Haydom inayounganisha Mikoa ya Singida na Manyara ni kiungo muhimu katika kusafirisha mazao ya wakulima na bidhaa za wafanyabiashara na inapita katika Hospitali ya Rufaa ya Haydom ambayo wananchi hufuata huduma kwa kukosa Hospitali ya Serikali katika Halmashauri.
Je, ni lini barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami ili kunusuru maisha ya wananchi wa Singida Kaskazini?

Name

Eng. Atashasta Justus Nditiye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Answer

NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Justin Joseph Monko, Mbunge wa Singida Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Singida – Ilongero – Mtinko - Nkugi na Kidarafa hadi Haydom ni barabara ya mkoa yenye urefu wa kilometa 93.4 ambapo kilometa 84.36 zipo mkoani Singida na kilometa 9.04 zipo katika mkoa wa Manyara. Barabara hii inahudumiwa na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS).
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa barabara hii kwa wananchi wa Mikoa ya Singida na Manyara kwa ajili ya usafirishaji wa abiria, mazao, bidhaa za biashara na pia wananchi wanaokwenda kupata huduma ya matibabu katika hospitali ya Haydom. Hivyo kwa umuhimu huo Serikali imekuwa ikiifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hii kila mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018 barabara hii ilitengewa kiasi cha shilingi bilioni 2.246 kwa ajili ya matengenezo mbalimbali. Aidha, Serikali imejenga jumla ya kilometa 8 kwa awamu kwa kiwango cha lami kuanzia Singida Mjini kuelekea Ilongero na jumla ya kilometa tano za barabara hii zimepangwa kujengwa kwa kiwango cha lami katika mwaka wa fedha 2018/2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa kipaumbele cha Serikali ni kuunganisha kwa barabara za kiwango cha lami makao makuu ya mikoa na nchi jirani na baadae barabara za mikoa zitafuata.