Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 11 Sitting 3 Works, Transport and Communication Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano 22 2018-04-05

Name

Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Primary Question

MHE. ANTHONY C. KOMU (K.n.y. MHE. ZITTO Z. R. KABWE) aliuliza:-
Mnamo tarehe 26 Julai, 2017, Mawaziri wa Uchukuzi wa Uganda, Burundi, Congo DRC na Tanzania walifanya mkutano katika Manispaa ya Ujiji-Kigoma na kuazimia kuwa kuanzia Januari, 2018, Bandari ya Kigoma itakuwa bandari ya mwisho kwa bidhaa ya Burundi na Mashariki ya DRC (Kigoma Port of Destination CIF Kigoma). Pamoja na Azimio hilo, mradi wa Bandari ndogo za Ujiji na Kibirizi zilipaswa kujengwa na kuiwezesha miradi kama ya Ujiji City-Great Lakes Trade and Logistics Centre:-
Je, Serikali mpaka sasa imefikia hatua gani ya kiforodha na kibandari kuiwezesha CIF-Kigoma?

Name

Eng. Atashasta Justus Nditiye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kabwe Ruyagwa Zitto, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba katika Mkutano wa Mawaziri wa Uchukuzi wa Uganda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Tanzania waliazimia kuwa kuanzia Januari, 2018 Bandari ya Kigoma itakuwa Bandari ya mwisho kwa bidhaa za Burundi na Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yaani Kigoma Port of Destination.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwa bandari hii pia ni muhimu sana kwa uchumi na ustawi wa Mkoa wa Kigoma na ndiyo inategemewa na wananchi wa Mkoa wa Kigoma na Mikoa ya jirani katika utaoji wa huduma ya usafirishaji wa bidhaa zinazopitia reli ya kati kutoka bandari ya Dar es Salaam kwenda nchi jirani za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tena kwa gharama nafuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kulitambua hili, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari - Tanzania katika mwaka wa fedha 2017/2018 imetenga fedha kwa ajili ya kuendeleza Bandari ndogo za Ujiji na Kibirizi ili zikikamilika ziwezeshe miradi kama vile Ujiji City –Great Lakes Trade and Logistics Centre. Zabuni za kumpata mkandarasi wa ujenzi wa bandari hizi zilitangazwa. Hata hivyo, kwa bahati mbaya hakuna mzabuni hata mmoja aliyejitokeza kuomba kazi hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Machi, 2018, TPA imetangaza upya zabuni hizo Kimataifa ili kumpata mzabuni atakayefanya kazi za upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na athari za kimazingira. Zabuni hizo zimefunguliwa tarehe 3 Aprili, yaani juzi na jumla ya makampuni 21 yameonyesha nia ya kufanya kazi hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa kazi inayoendelea ni kufanya tathmini ya wazabuni ili kumpata mzabuni anayefaa kufanya kazi hiyo. Ni matarajio yetu kuwa kazi itaanza mara baada ya kumalizika kazi ya tathmini na kumpata mkandarasi wa kufanya kazi hiyo na hivyo kunyanyua kiwango cha utendaji wa Bandari ya Kigoma.