Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 7 Sitting 51 Information, Culture, Arts and Sports Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo 419 2017-06-20

Name

Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Primary Question

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mawasiliano ya TBC Radio
kwenye maeneo ya Tarafa ya Amani Muheza ni hafifu.
• Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha mawasiliano ya redio na televisheni ya Kituo cha Taifa cha TBC?
• Je, ni lini Serikali itaboresha mawasiliano kwenye maeneo hayo ya milima ya Amani ya Vituo vya Taifa Redio na TBC ili wananchi waweze kunufaika na vipindi hivyo?

Name

Anastazia James Wambura

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajab, Mbunge wa Muheza, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa mawasiliano ya Redio na Televisheni ya Taifa (TBC) yanaimarishwa na kuwafikia wananchi katika mmaeneo yote ya nchi. Katika kutekeleza dhamira hiyo, Serikali kila mwaka imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kuimarisha miundombinu na usikivu wa redio na televisheni ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuboresha usikivu wa redio za Shirika katika maeneo ya mipakani mwa nchi ambayo ni Kakonko, Tarime, Rombo, Longido na Nyasa, na utekelezaji wa mradi huo unaendelea. Aidha, katika hatua ya kuhakikisha changamoto ya usikivu wa redio za Shirika inapatiwa ufumbuzi kwa kiwango kikubwa, Serikali imeendelea kuimarisha bajeti ya upanuzi wa usikivu wa TBC, ambapo katika mwaka 2017/2018 shilingi bilioni tatu zimetengwa ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni mbili ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2016/2017, ambapo kiasi cha shilingi bilioni moja zilitengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uimarishaji wa usikivu wa Redio na Televisheni ya Taifa ni wa hatua kwa hatua, hivyo Serikali itaendelea kutekeleza azma hii katika maeneo ambayo kuna usikivu hafifu kwa kuendelea kutenga fedha kila mwaka.