Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 9 Sitting 9 Water and Irrigation Maji na Umwagiliaji 113 2017-11-17

Name

Hawa Mchafu Chakoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:-
Kwa muda mrefu chanzo cha maji cha Ruvu Chini na Ruvu Juu kimekuwa chanzo pekee cha maji katika Mkoa wa Pwani. Lakini kimsingi chanzo hicho hakitoshelezi mahitaji na hivyo kushindwa kumaliza tatizo la maji.
Je, ni lini Serikali itatumia chanzo cha maji cha Mto Rufiji kuwapatia maji safi na salama wananchi hususan wa Wilaya ya Rufiji, Kibiti, Mkuranga na Kisarawe?

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika,kwa Niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Kuanzia mwaka 2005 hadi 2007 Serikali ilifanya uchunguzi wa vyanzo 26 vya maji kwa ajili ya matumizi ya Jiji la Dar es Salaam na Miji ya Kibaha na Bagamoyo kwa miaka 2025 hadi 2032. Uchunguzi huo ulibaini kuwa wakati ule vyanzo vya maji vya mto Ruvu na visima vya Kimbiji na Mpera vilikuwa vinatosha kwa matumizi ya Jiji la Dar es Salaam na maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Pwani hadi mwaka 2032. Chanzo cha maji cha Mto Rufiji hakikuchaguliwa wakati huo kwa sababu ilionekana gharama za kusafisha na kusafirisha maji kutoka Mto Rufiji hadi Dar es Salaam zilikuwa kubwa ukilinganisha na vyanzo vingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati uchunguzi huo unafanyika, Serikali ilifanya uchunguzi wa vyanzo mbadala kwa ajili ya miji ya Utete, Ikwiriri, Mkuranga na Kisarawe. Uchunguzi ulibaini kuwa miji hiyo inaweza kupata maji ya visima. Miradi mikubwa ya visima ilitekelezwa katika miji hiyo na kunufaisha wakazi wa maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukidhi mahitaji ya maji kwa Jiji la Dar es Salaam pamoja na maeneo ya Mkoa wa Pwani hususan Wilaya za Rufiji, Kibiti, Mkuranga na Kisarawe, Serikali imeanza taratibu za kumwajiri mtaalam mshauri kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na utayarishaji wa vitabu kwa kutumia chanzo cha Mto Rufiji. Kazi hiyo inatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2018/2019. Ahsante.