Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 8 Sitting 6 Home Affairs Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi 76 2017-09-12

Name

Kasuku Samson Bilago

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Buyungu

Primary Question

MHE. KASUKU S. BILAGO aliuliza:-
Jimbo la Buyungu Wilayani Kakonko linapakana na nchi ya Burundi, hivyo raia wa nchi hizi mbili wanafanya baadhi ya shughuli za kibiashara na kijamii kwa kushirikiana kwa muda mrefu hata kabla ya Burundi kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
(a) Je, ni lini Serikali itafungua Ofisi ya Uhamiaji katika kijiji cha Muhange iliyofungwa bila sababu za msingi?
(b) Je, kwa nini Warundi wakija kufanya biashara kwenye masoko ya ujirani mwema au kulima mashamba hukamatwa na kufungwa jela?
(c) Je, kwa nini Warundi 254 waliofungwa kwa makosa kama hayo wasirudishwe kwao ili kupunguza msongamano magerezani?

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kasuku Samson Bilago, Mbunge wa Buyungu, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Uhamiaji katika Kijiji cha Muhange ilifungwa kutokana na sababu za kiusalama baada ya nchi jirani ya Burundi kuingia katika machafuko miaka ya 1990. Hata hivyo Serikali itaangalia endapo mazingira ya sasa yanaruhusu kujenga Ofisi hiyo.
(b) Mheshimiwa Spika, Idara ya Uhamiaji inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazoruhusu wageni kuingia nchini, kuishi na kufanya kazi. Hivyo, wageni wote waingiapo nchini wakiwemo raia wa Burundi wanapaswa kuafuata sheria na taratibu zilizopo.
(c) Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna msongamamno wa wafungwa katika Magereza yetu nchini kutokana na sababu mbalimbali ambapo kwa sasa kuna jumla ya wafungwa 725, raia wa Burundi katika Mkoa wa Kigoma ambao wamefungwa kwa makosa mbalimbali.
Hata hivyo, ipo sheria inayoruhusu kumrudisha mfungwa kwao kwa yule ambaye sio Mtanzania. Sheria hiyo inaitwa The Transfer of Prisoners Act (No. 10) of 2004 na Kanuni zake (The Transfer of Prisoners Regulations of 2004).
Mheshimiwa Spika, sheria hii inatumika pale tu mfungwa wa nchi nyingine anapoomba kumalizia sehemu kifungo chake kwenye nchi yake ya asili.