Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 7 Sitting 1 Natural Resources and Tourism Wizara ya Maliasili na Utalii 02 2017-04-04

Name

Amina Saleh Athuman Mollel

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. AMINA S. MOLLEL aliuliza:-
Wakazi wanaoishi katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro wamekatazwa kulima kwenye maeneo wanayoishi kwa mujibu wa sheria hali iliyochangia wakazi wengi katika eneo hilo ambao ni wafugaji kukabiliwa na njaa pamoja na umaskini mkubwa wa kipato:-
Je, ni lini Serikali itarekebisha Sheria ya Mamlaka ya Hifadhi (Ngorongoro Conservation Area Act), 1959 Revised Edition, 2002) ili wananchi wa maeneo haya wapate maeneo kwa ajili ya shughuli zao za kilimo na ufugaji?

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Saleh Mollel, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha Hifadhi ya Ngorongoro, Sheria ya Kuhifadhi Eneo la Ngorongoro ya mwaka 1959 iliyopitiwa mwaka 2002 (The Ngorongoro Conservation Area Act 1959, R.E 2002) wananchi wakaazi katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro hawaruhusiwi kulima bali kufuga peke yake.
Mheshimiwa Spika, kutokana na zuio la kisheria la kulima, wakazi wa eneo la Ngorongoro ambao kwa asili yao ni wafugaji, wamekuwa wakitengewa bajeti ya kununulia mahindi ambapo takribani tani 3,600 hugawiwa bila malipo kila mwaka kwa matumizi ya chakula hususan kwa wale uwezo, mahindi hayo huuzwa kwao kwa bei pungufu ya bei ya soko.
Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto ya chakula, mnamo mwaka 2007, mamlaka ilianza mchakato wa kupata maeneo ya kilimo nje ya hifadhi kwa kutenga bajeti na kuwezesha mradi wa JEMA. Malengo mawili ya mradi wa JEMA ulioko katika Kata ya Oldonyosambu ni haya yafuatayo:-
(a) Kuwaondoa wahamiaji walioingia ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro ambao hawakuwa wakazi halali kwa kuzingatia kwamba wakazi halali ni wale waliokuwepo pamoja na uzao wao wakati eneo la Hifadhi ya Ngorongoro lilipotangazwa rasmi mwaka 1959.
(b) Kutoa fursa kwa wakazi wenyeji na halali ambao wangependa kufanya shughuli za kilimo na ufugaji nje ya hifadhi.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mradi huu kuendelea, tathmini ya awali inaonesha upungufu kwa baadhi ya waliohamishiwa eneo la mradi kuuza maeneo waliyopewa na kurejea kinyemela ndani ya hifadhi. Kutokana na upungufu huo, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kushirikiana na uongozi wa Wilaya ya Ngorongoro, inaendelea kuchukua hatua ya kuzuia uuzwaji wa maeneo katika eneo la mradi.
Aidha, kwa kuwa maeneo yaliyopatikana hapo awali hayakuweza kutosheleza mahitaji, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kushirikiana na wadau wengine inaendelea kutafuta maeneo mengine yatakayotumika kwa kilimo.
Mheshimiwa Spika, sheria iliyoanzisha eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ilianza kutumika zaidi ya miaka 50 iliyopita na Serikali iko kwenye maandalizi ya awali ya kufanya marekebisho yake. Ni muhimu kuzingatia kwamba, katika marekebisho hayo Serikali itaweka msisitizo zaidi katika kuboresha shughuli za uhifadhi wa eneo la Ngorongoro ili libakie katika orodha ya maeneo ya urithi wa dunia.