Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 5 Sitting 1 Good Governance Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu 02 2016-11-01

Name

Hafidh Ali Tahir

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dimani

Primary Question

MHE. HAFIDH ALI TAHIR aliuliza:-
Chaguzi zetu zimekuwa zikikumbwa na matatizo mengi yanayosababisha upotevu wa fedha nyingi za Taifa jambo linaloweza kuepukika kwa faida ya Watanzania mathalani inapotokea mshindi wa uchaguzi wa Jimbo wa chama fulani amefariki hurudiwa badala ya nafasi hiyo kuchukuliwa na mshindi wa pili ndani ya chama hicho.
(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka utaratibu kuwa pindi mshindi wa jimbo kupitia chama fulani anapofariki mshindi wa pili ndani ya chama apewe nafasi aliyoiacha marehemu badala ya kurudia uchaguzi?
(b) Je, Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka kuondoa utaratibu wa kusimamisha uchaguzi mkuu wakati mgombea anapofariki?

Name

Dr. Abdallah Saleh Possi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hafidh Ali Tahir, Mbunge wa Dimani lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria za uchaguzi pamoja na mfumo wa uchaguzi tulionao unamwelekeza mpiga kura kumpigia mtu (mgombea) na siyo chama kama ilivyo katika mifumo mingine ya uchaguzi ya kupigia chama. Hivyo, kwa sasa Serikali itaendelea kutumia utaratibu uliopo, kwa sababu mshindi wa pili atakayechukuliwa kujaza nafasi ya wazi, atakuwa hajachaguliwa na wananchi wote nchini au jimbo au kata husika, bali wanachama wachache wa chama hicho.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya sasa ya Uchaguzi, Sura ya 343 inaelekeza kusimamisha uchaguzi mkuu nchi nzima anapofariki mgombea Urais au Makamu wa Rais. Anapofariki mgombea Ubunge au Udiwani, uchaguzi mkuu nchi nzima huendelea, isipokuwa katika jimbo au kata husika ambayo mgombea amefariki. Hata hivyo, sheria ya uchaguzi inaweza kufanyiwa marekebisho kwa kuzingatia wakati uliopo, mazingira halisi ya nchi, tafiti na tathmini za uchaguzi zinazofanyika na jambo hili linaweza kujadiliwa pia.