Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 4 Sitting 6 Natural Resources and Tourism Wizara ya Maliasili na Utalii 74 2016-09-14

Name

Susan Limbweni Kiwanga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Mlimba

Primary Question

MHE. SUSAN L. KIWANGA aliuliza:-
Serikali imetwaa maeneo ya vijiji katika Kata za Idete, Namwala, Mofu, Mbinga, Igima, Mchombe, Mngeta, Kalengakelu, Mlimba, Kamwene, Chita na Utengule kwa madai kwamba ni maeneo ya hifadhi bila kuwashirikisha wananchi, jambo ambalo limefanya wananchi kushindwa kuendeleza shughuli zao za kilimo na ufugaji na hivyo kuendelea kuwa maskini.
Je, Serikali itakuwa tayari kushirikisha wananchi ili kuweka mipaka kati ya maeneo ya kilimo na ufugaji na yale ya Hifadhi ya Taifa ili kuondoa mgogoro wa ardhi uliopo hivi sasa kwa wananchi kukosa maeneo ya kilimo na malisho ya mifugo?

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu haijawahi kutwaa na haina utaratibu wa kutwaa maeneo ya vijiji na kuyafanya kuwa maeneo ya hifadhi bila ya kuwashirikisha wananchi. Aidha, sehemu ya maeneo ya vijiji vilivyoko ndani ya kata 12 zilizotajwa yamo ndani ya eneo la Hifadhi ya Ramsar ya Bonde la Kilombero iliyotambulika na kuorodheshwa mwaka 2002.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Ramsar la Bonde la Kilombero ni muendelezo wa hifadhi ulioanza na Pori Tengefu la Kilombero lililoanzishwa kwa Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori, Sura ya 302 ya mwaka 1952 kupitia Tangazo la Serikali Namba107. Pori hili lilirithiwa na Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Namba12 ya mwaka 1974 na kuboreshwa na Sheria Namba 459 ya mwaka 1977 baada ya taratibu zote za kisheria kukamilika ikiwemo ushirikishaji wananchi. Aidha, eneo hili ambalo ni chanzo kikubwa cha maji na lenye uwepo wa viumbe adimu duniani lina ukubwa wa kilometa za mraba 7,967.35 sawa na hekta 795,735 sifa ambazo zinalifanya kuwa eneo la tatu kwa ukubwa lenye umuhimu wa Kimataifa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya ardhi liliyopo baina ya wananchi na vijiji katika kata zilizotajwa ambavyo vilianzishwa baada ya kuanzishwa kwa Pori Tengefu la Kilombero imetokana na hatua mbalimbali za ukiukaji wa sheria, kanuni na taratibu. Aidha, katika kutatua migogoro hiyo, Serikali inaendelea kutekeleza yafuatayo:-
(a)Kupitia Mradi wa KILORWEMP unaotekelzwa chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii; kupitia upya mipaka, kuweka alama, kuchora ramani na kutunza kumbukumbu kwa njia za kawaida na kielektroniki.
(b)Kupitia mpango wa upimaji ardhi za vijiji vya Wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi unaosimamiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; kukamilisha upimaji na urasimishaji wa ardhi ambapo mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji itaandaliwa na wananchi na watamilikishwa ardhi kisheria.
(c)Kupitia Kamati Maalum ya Kitaifa iliyoundwa kushughulikia migogoro ya rdhi nchini; kufika katika maeneo ya Ramsar na Pori Tengefu la Kilombero na kutekeleza majukumu yake katika kutatua migogoro kwa kuwashirikisha wananchi kama ilivyo kwa utekelezaji wa hatua zingine nilizozitaja hapo juu.