Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 3 Sitting 38 Natural Resources and Tourism Wizara ya Maliasili na Utalii 322 2016-06-07

Name

Maria Ndilla Kangoye

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARIA N. KANGOYE aliuliza:-
Sekta ya Utalii ni Sekta inayotegemewa kuliingiza Taifa mapato kwa sababu ya vivutio vingi tulivyojaliwa Tanzania:-
(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kutekeleza ahadi iliyopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2016 - 2020 katika kuongeza bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii?
(b) Je, ni nini mkakati wa Serikali kukiimarisha Chuo cha Utalii ili kutoa mafunzo ya Hoteli na Utalii katika ngazi ya Stashahada ili kuongeza ubora wa Watumishi wa huduma za ukarimu na utalii?
(c) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweka mazingira bora ya kuwezesha vijana kuanzisha makampuni ya kutembeza watalii katika maeneo mbalimbali ya utalii?

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maria Ndilla Kangoye, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2016 -2020, katika Ibara ya 29(c) inaainisha azma ya Chama cha Mapinduzi kusimamia Serikali katika utekelezaji wa mikakati ya kukuza utalii nchini kwa kuhakikisha kwamba bajeti ya Sekta ya Utalii inaongezeka ili kuutangaza utalii ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mkakati huo, Wizara yangu kupitia Bodi ya Utalii na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania imetenga jumla ya sh. 2,730,188,676/= kwa ajili ya shughuli za utangazaji kwa mwaka wa fedha 2016/2017, hii ikiwa ni ongezeko la asilimia 14.7 ikilinganishwa na mwaka 2015/2016. Serikali itaendelea kuboresha utekelezaji wa ahadi hii kwa kushirikisha pia wadau mbalimbali wa maendeleo na vyanzo vingine kama inavyoainishwa na mpango wa maendeleo wa miaka mitano 2016/2017 – 2020/2021.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali katika kukiimarisha Chuo cha Utalii katika Kampasi zake zote tatu za Bustani, iliyoko Dar es Salaam; ya Temeke iliyoko Dar es Salaam pia na ya Arusha. Ni pamoja na kuongeza idadi na umahiri wa wakufunzi, kuboresha upatikanaji wa vifaa mbalimbali vya kufundishia na kuboresha miundombinu ya chuo katika kampasi zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mipango ya hivi karibuni Chuo cha Utalii kitaboresha utoaji wa mafunzo katika Tasnia ya Ukarimu (Hospitality) na Utalii (Tourism) katika ngazi ya Shahada.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Chuo cha Utalii kwa kushirikiana na Chuo cha Vancouver Island University cha Canada kupitia Mradi wa ISTEP chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kitaanzisha mafunzo ya uongozi katika ngazi ya Shahada kuanzia mwezi Septemba, 2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uimarishaji wa miundombinu, Wizara yangu imetenga jumla ya shilingi milioni 500 katika mwaka wa fedha 2016/2017 ili kukamilisha ujenzi wa jengo la Utalii (Utalii House) Phase II katika Kampasi ya Bustani ya Chuo cha Utalii, Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mazingira bora ya kuwezesha vijana kuanzisha makampuni ya kutembeza watalii katika maeneo mbalimbali ya utalii; Serikali itaendelea kwa msisitizo zaidi kushirikisha sekta binafsi ili kuwashauri vijana wajiunge katika vikundi na kuwapa elimu ili waanzishe na kushiriki kwa tija zaidi katika biashara hii kwa maslahi yao na kwa maslahi ya Taifa. Serikali pia itapitia masharti yote yaliyopo kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu ili kuona kama kutakuwa na uhitaji wa kuyafanya masharti hayo kuwa rafiki zaidi kwa vijana wenye nia thabiti ya kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa Taifa kupitia shughuli za uongozaji watalii.