Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 3 Sitting 44 Health and Social Welfare Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto 376 2016-06-16

Name

Joseph Osmund Mbilinyi

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbeya Mjini

Primary Question

MHE. CATHERINE V. MAGIGE (K.n.y. MHE. JOSEPH O. MBILINYI) aliuliza:-
Je, ni lini jengo la maabara ya mionzi linalojengwa kwa muda mrefu sasa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mbeya litakamilika na vipimo vya CT-Scan na MRI-Scan vitaletwa na kuanza kazi?

Name

Ummy Ally Mwalimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Osmund Mbilinyi, niruhusu nitumie Bunge lako Tukufu kuwatakia kheri watoto wote wa Tanzania, watoto wote wa Afrika kwa kuwa leo ni siku ya Mtoto wa Afrika. Kaulimbiu ya mwaka huu tunasema „Ubakaji na Ulawiti kwa Watoto Vinaepukika, Chukua Hatua Kuwalinda Watoto‟.
Mheshimiwa Naibu Spika, Nataka kuwathibitishia watoto wa Tanzania kwamba Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha wabakaji na walawiti wa watoto wanafikiwa na mkono wa dola na kila mbakaji ajiandae kutumikia kifungo cha miaka 30. Tutawalinda watoto wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nitumie Bunge lako Tukufu kuwaomba Waheshimiwa Wabunge kuendelea kuwahamasisha wazazi, walezi, kuongeza jitihada za kuwalinda watoto wetu kwa sababu 48% ya ubakaji na ulawiti unatokea katika nyumba zetu. Kwa hiyo, nyumba zetu siyo salama kwa watoto wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, sasa napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Osmund Mbilinyi, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Afya ilianza mradi wa ujenzi wa jengo…
NAIBU SPIKA: Mbeya Mjini, Mheshimiwa Waziri.
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Osmund Mbilinyi, Mbunge wa Mbeya Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ilianza mradi wa ujenzi wa Jengo la X-Ray katika Hospitali ya Rufaa Mbeya tarehe 9 Novemba, 2010 lengo likiwa ni kuboresha huduma za uchunguzi katika hospitali hii inayohudumia wakazi wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini. Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2013/2014 hadi 2014/2015 kiasi cha Sh.614,670,000/= kilitolewa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi katika mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2015/2016 kiasi cha shilingi bilioni 8 kilitengwa, fedha ambayo mpaka sasa haijatolewa. Hata hivyo, Wizara bado ina nia ya kukamilisha ujenzi wa mradi huu, hivyo katika mwaka wa fedha 2016/2017 Wizara imetenga kiasi cha shilingi bilioni 5 katika bajeti ya maendeleo ambazo zitatumika kama ifuatavyo:-
(i) Shilingi bilioni 3 zitatumika kuendeleza ujenzi pamoja na kulipa deni lililobaki kwa mkandarasi aliyekuwa anajenga; na
(ii) Shilingi bilioni 2 zitatumika kununua vifaa tiba zikiwemo CT-Scan na MRI.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni matarajio yangu kwamba ujenzi huu utakamilika mwaka ujao wa fedha 2016/2017 pamoja na kusimika vifaa.